• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 2:32 PM
Kenya inaelewa lugha ya nishati safi – Ruto

Kenya inaelewa lugha ya nishati safi – Ruto

Na PAULINE ONGAJI akiwa BERLIN, UJERUMANI

RAIS William Ruto ametangaza kwamba mipango ya kutekeleza sheria za leseni za kudhibiti uzalishaji gesi ya dioksidi ya kaboni (carbon credits) ambayo inashughulikiwa na bunge itatekelezwa katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Alisema haya alipokuwa akihutubu kwenye Kongamano la Berlin kuhusu Kawi (Berlin Energy Transition Dialogue ambapo aliangazia umuhimu wa kubadilisha matumizi ya kawi kutoka nishati ya visukuku hadi nishati jadidifu, kama mbinu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Huku akiipongeza Kenya kwa kupiga hatua katika harakati za kutekeleza mabadiliko haya, Rais Ruto alitoa mwito kwa viongozi duniani kushughulikia suala la uzalishaji wa gesi ya kdioksidi ya kaboni kwa kina. “

“Hii leo barani Afrika, tunakumbwa na changamoto zinazotokana na makali ya mabadiliko ya tabianchi, licha ya kuwa tunazalisha kiwango kidogo zaidi cha gesi hii inayochangia kiwango cha joto ulimwenguni. Pia, katika masuala ya ufikiaji nishati, zaidi ya Waafrika milioni 600 wanaathirika pakubwa,” alisema.

Lakini licha ya changamoto hizi, Rais Ruto alisema kwamba bara hili bado lina uwezo mkuu wa kuchangia pakubwa katika uzalishaji wa nishati jadidifu. “Kinyume na bara Ulaya, uwezo wa Afrika ni mkubwa kwani ina rasilimali nyingi za kuzalisha nishati ya sola na ile ya upepo,” alisema, huku akiongeza kwamba pia Afrika ina kiwango kikubwa cha madini, baadhi yao yanayohitajika katika uzalishaji wa nishati jadidifu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ujerumani Bi  Annalena Baerbock alisema kwamba mbali na kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi, uzalishaji wa nishati jadidifu ni muhimu kwani inatoa nafasi za ajira.

Aliipongeza Kenya kwa kuwa kupiga hatua katika harakati za kuafikia uzalishaji wa nishati jadidifu huku akisema kwamba hii inatia changmoto kwa mataifa hasa yaliyostawi pia kuiga mfano huo.

Mipango ya awali ya Rais Ruto kuungana na Bi Baerbock kwa kikao na wanahabari ilivunjiliwa mbali.

Kongamano la The Berlin Energy Transition Dialogue huandaliwa na serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na mashirika mengine yanayohusiana na nishati jadidifu nchini humo. Katika konagmano la mwaka huu, zaidi ya wageni 2000 kutoka zaidi ya mataifa 100 wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya siku mbili, huku mawaziri na wajumbe wakuu kutoka nchi tofauti wakitarajiwa kujadiliana na wawakilishi wa wafanyabiashara, wanasayansi na mashirika ya kijamii.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wakongamana Thika kujazwa hekima

Ichung’wah akana kuhusika na uvamizi wa shamba la...

T L