• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
IEBC ielimishe Wakenya jinsi ya kutimua viongozi

IEBC ielimishe Wakenya jinsi ya kutimua viongozi

Na LEONARD ONYANGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) leo inaanza shughuli ya kuhamasisha Wakenya kuhusiana na masuala mbalimbali ya uchaguzi huku nchi ikijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wapigakura watapata fursa ya kuchunguza ikiwa taarifa kuwahusu zilizomo katika daftari la wapigakura ni sahihi wakati wa shughuli hiyo itakayokamilika Juni 20, mwaka huu.Wananchi waliohitimu ambao si wapigakura pia watapata fursa ya kujisajili.

Wakenya wanafaa kutumia fursa hiyo kujisajili kuwa wapigakura ili watekeleze haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wawapendao.Shughuli ya kusajili wapigakura kwa wingi itafanyika kati ya Januari na Februari mwaka ujao, lakini kutokana na tishio la virusi vya corona huenda idadi ya watu watakaojitokeza kujisajili wakati huo ikawa ndogo mno.

Kabla ya Uchaguzi wa 2017, IEBC ililenga kusajili wapigakura wapya milioni sita. Lakini ilifanikiwa kusajili wapigakura wapya milioni 3.8 pekee.Takwimu za Sensa ya 2019 zinaonyesha kuwa vijana milioni tano waliokuwa na umri wa kati ya miaka 13 na 17 mnamo 2017, sasa wamehitimu kuwa wapigakura kufikia 2022.

Vijana hao wanafaa kuhamasishwa kujitokeza wiki hii kujisajili kuwa wapigakura badala ya kungojea Januari 2022.Mbali na kuwahamasisha wananchi kuhusu masuala ya kupiga kura, IEBC pia inafaa kutumia wiki hii kuwaelimisha Wakenya kuhusu mamlaka waliyopewa na Katiba kuhusu namna ya kuwaadhibu viongozi wanaowachagua.

Katiba, kwa mfano, inaruhusu wapigakura kumtimua mbunge wao ambaye amethibitishwa na mahakama kukiuka Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili.Katiba inasema kuwa mbunge ambaye amethibitishwa na mahakama kuwa amefuja fedha za umma anastahili kutimuliwa na wapigakura wake.Mchakato wa kumtimua mbunge unafaa kuanzishwa baada ya Mahakama Kuu kumpata na hatia ya kukiuka maadili au kufuja fedha za umma.

Washindani wake waliobwagwa katika uchaguzi hawafai kuanzisha mchakato wa kumng’oa mbunge.Tangu kuanza kutekelezwa kwa Katiba ya 2010, magavana watatu; Babayao Waititu (Kiambu), Mike Mbuvi Sonko (Nairobi) na Mohamed Mohamud (Wajir) wametimuliwa afisini baada ya kupatikana na sakata mbalimbali, ikiwemo matumizi mabaya ya mamlaka na wizi wa fedha za umma.

Lakini hakuna hata mbunge, seneta au diwani mmoja ambaye ametimuliwa licha ya kuhusika katika visa vya ukiukaji wa maadili.Vifungu vya 27, 28 na 29 vya Sheria ya Serikali za Kaunti vinaruhusu wapigakura kumtimua diwani wao kwa kukiuka maadili.

Ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ambazo zimekuwa zikitolewa kila mwaka zimefichua uozo katika usimamizi wa Hazina ya Fedha za Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF), tumeshudia wabunge na madiwani wakipigana bungeni, kumekuwa na madai ya madiwani, wabunge na maseneta kuchukua hongo chooni ili kutupilia mbali au kupitisha ripoti fulani Bungeni.

Lakini hawachukuliwi hatua labda kwa sababu wapigakura hawajui utaratibu.Baada ya kupitisha sheria iliyoruhusu wapigakura nchini Uingereza kutimua wabunge wao mnamo 2015, wabunge kadhaa wamejipata taabani.

Mmoja wa wabunge waliotimuliwa na wapigakura, alipatikana na hatia ya kusema uongo kwamba gari lake lilikuwa likiendeshwa na mtu mwingine wakati wa kupata ajali.

  • Tags

You can share this post!

Raia waandamana kushinikizaBuhari ang’atuke mamlakani

Magavana sasa tumbojoto kuhusu miradi iliyokwama