• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Jaji akataa malalamiko kuhusu lugha

Jaji akataa malalamiko kuhusu lugha

Na BRIAN OCHARO

KESI dhidi ya raia wa kigeni ambao walishtakiwa kwa madai ya ulanguzi wa dawa ya kulevya, aina ya heroini ya thamani ya Sh1.3 billioni, itaendelea kusikilizwa licha ya mshtakiwa kulalamika kwamba haelewi lugha inayotumiwa.

Jaji Anne Ong’injo wa Mahakama Kuu mjini Mombasa alikataa ombi la raia wa Iran, Pak Abdolghaffer, kutaka mkalimani mwingine aletwe akidai haelewi lugha ya Kiurdu inayotumiwa katika kesi hiyo.

Jaji Anne Ong’injo alisema suala la lugha lingesemwa katika hatua za awali kabla ya shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wake.

Jaji huyo alishikilia kuwa Bw Abdolghaffer hakuwa na nia njema kwa kuomba kuletewa mkalimani wa lugha ya Kiparsi ilhali amekuwa akiskiza kesi hiyo kupitia kwa mkalimani wa lugha ya Kiurdu tangu mwanzoni.

“Haiwezi kuwa kweli kwamba karibu miaka saba raia huyo wa Iran sasa anadai kwamba haelewi lugha ya Kiurdu,” alisema.

Zaidi ya hayo, Jaji Ong’injo alibainisha kuwa Bw Abdolghaffer hakuwasilisha malalamiko yoyote katika hatua za awali ya kesi hiyo kwamba haelewi lugha hiyo au kwamba Bw Amin Ahmed, ambaye amekuwa akitoa huduma za ukalimani kwa lugha ya Kiurdu, alitafsiri visivyo.

Wakati akitaka kusitisha kesi hiyo, Bw Abdolghaffer alilalamika kuwa ingawa anazungumza Kifarsi na Kiajemi, mahakama ya hakimu ilipuuza ombi lake la kutaka kuwa na mkalimani wa lugha hizo mbili.

“Hii imekiuka haki yangu na kusababisha makosa mengi ambayo yanaweza kufanya nikose kufanyiwa haki,” akasema kupitia kwa wakili Jacqueline Waihenya.

Kiongozi wa mashtaka katika kesi hiyo, Bw Alexander Muteti alikuwa amepinga ombi hilo.

“Wakati maelezo yake yakichukuliwa katika kituo cha polisi cha bandarini, mkalimani alikwenda pale na akafanya tafsiri kutoka Kiingereza hadi Kiurdu. Bw Abdolghaffer alizungumza Kiurdu kwa ufasaha sana,” Bw Muteti alisema.

Bw Abdolghaffer ameshtakiwa kuwa pamoja na wengine 11 walihusika kwa ulanguzi wa mihadarati iliyonaswa katika Bahari Hindi ikiwa imefichwa kwenye meli Amin Darya ambayo pia inajulikana kama Al Noor.

Serikali inadai kuwa washukiwa hao walitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya Julai 2 na 18, 2014 katika bandari ya Kilindini.

Washukiwa wengine ni mwanasiasa wa Mombasa Maur Bwanamaka, Yousuf Yaqoob, Yakoob Ibrahim, Saleem Muhammad, Bhatti Abdul Ghafour, Baksh Moula, Muhammed Saleh, Mohamed Osman Ahmed, na Khalid Agil.

Serikali ya Pakistani imeelezea wasiwasi juu ya kucheleweshwa kwa kesi hiyo dhidi ya raia wake sita na inataka ikamilike ili washukiwa hao wajue hatima yao badala ya kuwekwa katika mashaka katika gereza la Shimo La Tewa.

You can share this post!

Wageni Pwani waonywa kuwa makini baharini

Wasiwasi migawanyiko itamponza Raila, ODM

T L