• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Wasiwasi migawanyiko itamponza Raila, ODM

Wasiwasi migawanyiko itamponza Raila, ODM

Na STEPHEN ODUOR

BAADHI ya wanachama wa ODM katika Kaunti ya Tana River, wameonya kuwa umaarufu wa chama hicho na kiongozi wake, Bw Raila Odinga, unahatarishwa na migawanyiko inayoendelea chamani.

Baadhi yao wametishia kuhama chama hicho wakidai kuna ubaguzi katika uongozi.

Walalamishi wamedai kuwa, wanasiasa matajiri wameteka chama hicho na kuweka viongozi ambao ni wandani wao pekee.

Wakiongozwa na Bw James Rashid, wamedai kuwa Bw Oscar Kasema, ambaye jina lake liliwasilishwa kwa Bodi ya Kitaifa ya Chama ili awe mwenyekiti Tana River, alijisajili chamani miezi miwili iliyopita.

Kulingana naye, katiba ya chama inahitaji mtu awe mwanachama wa daima kwa angalau miezi sita ndipo akubaliwe kuwania uongozi chamani.

“Tumejaribu kutatua suala hili na viongozi wa bodi ya kitaifa ya uchaguzi lakini tunapuuzwa,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kaseme alipuuzilia mbali madai hayo na kuwataka waache kujichukulia kuwa muhimu zaidi kuliko wanachama wengine.

“Sote tulikubaliwa kuwania nafasi chamani. Niliwania nikashinda. Wanachama walinichagua kwa hivyo inafaa waache vitimbi vyao, waungane nasi kukuza chama,” akaeleza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ODM, Bi Catherine Mumma, alishauri wanachama ambao wana malalamishi wayapeleke kwa bodi yake jinsi inavyohitajika kwa sheria za chama.

Wanaolalamika walidai pia kuwa naibu mwenyekiti, Bw Ali Balagha, ni mgeni chamani kwani aliingia majuzi, na hivyo hakustahili kupewa nafasi ya uongozi ila awe katika kamati ya muda.

Mratibu wa chama hicho, Bw Ernest Akumu, alidai kuwa Bw Balagha alijiunga na ODM mnamo Septemba kwa hivyo angefaa tu kuwa mwanachama katika kamati ya muda na wala si kushikilia wadhifa wa naibu mwenyekiti.

Mivutano hiyo ya uongozi imegawanya wanachama na kutatiza shughuli za kusajili wanachama wapya kabla uchaguzi ujao.

Mizozo ilikuwa imeanza Septemba 2020, wakati wanachama waligawanyika pande tatu, upande mmoja ukiegemea Gavana Dhadho Godhana, mwingine kwa Mwenyekiti Adam Dhidha na waliosalia wakiegemea kwa kiongozi wa wanawake chamani, Alfelt Abio.

Hali hiyo ilimlazimu Katibu Mkuu Edwin Sifuna kufunga afisi ya chama Tana River hadi watatue tofauti zao.

Bi Mumma aliingilia kati baadaye, na kupatanisha pande hizo tatu ambazo zilikubaliana kutafuta suluhu.Walikubaliana kuunda afisi ya muda ya uongozi, lakini hilo linaonekana kutatizika.

You can share this post!

Jaji akataa malalamiko kuhusu lugha

Mlipuko usiku waibua hofu kijijini Lamu

T L