• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Jaji ataka mkewe alipwe mshahara akiwa Jaji Mkuu

Jaji ataka mkewe alipwe mshahara akiwa Jaji Mkuu

Na RICHARD MUNGUTI

Jaji David Njagi K Marete, aliyehojiwa jana kwa nafasi ya Jaji Mkuu, aliomba serikali iwe ikimlipa mkewe mshahara kwa kumsaidia kutokana na ulemavu alionao.

Jaji Marete, 61, alisema anahitaji msaada wa mkewe anapotekeleza majukumu yake kazini.

“Siwezi kuishi peke yangu. Nahitaji msaidizi anayenielewa barabara na ambaye hatachoka nami,” alifichua Jaji Marete huku akilikabidhi jopo la tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama (JSC) cheti kinachothibitisha ulemavu alio nao.

Jaji huyo alisema inabidi mkewe aliyestaafu baada ya kutumikia serikali miaka 38 aandamane naye.

Jaji huyo anayeomba ateuliwe kumrithi Bw David Maraga kuwa Jaji Mkuu wa tatu baada ya kuzinduliwa kwa katiba ya 2010 alisema “akiachwa peke yake hawezi kujimudu.”

Licha ya ulemavu alioueleza kwa herufi “INFJ”, Jaji Marete alijipigia debe kuwa mwaniaji maalum ambaye “tu peke yake anastahili kuteuliwa kutokana na weledi alionao katika taaluma ya sheria na ushupavu katika masuala ya usimamizi.”

Alisababisha kicheko alipodai kuwa “ siku ile alipozaliwa ni muuguzi aliyepokea kutoka tumboni mwa mama yake aliyelia badala yake (marete).” ,

Na wakati huo huo Jaji Marete alifichua kuwa ndiye amejiajiria dereva anayempeleka kazini na kumrudisha.

“Alisema alikosana na madereva kutoka idara ya polisi kwa vile hawamuelewi kwa sababu ya ulemavu alionao,” Jaji Marete alisema.

Jaji Marete anayehudumu katika mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi alisema endapo atateuliwa kuwa Jaji Mkuu atatumia ujuzi alionao kuleta mshikamano na ushirikiano kuboresha utenda kazi katika idara ya mahakama.

You can share this post!

Msako wa baharini wapunguza samaki

Nikipata fursa kuwa Rais sitamhangaisha naibu wangu –...