• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
‘Jinsi Sharon alivyosafirishwa kuuawa’

‘Jinsi Sharon alivyosafirishwa kuuawa’

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu ilifahamishwa Alhamisi kuwa aliyekuwa msaidizi wa Gavana wa Migori Okoth Obado, aliwabeba kwa gari, mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno na mtu mwingine kutoka hoteli ya Graca, siku aliyotoweka mwanachuo huyo na kisha kupatikana ameuawa.

Afisa wa Polisi Konstebo Willy Okoti alimweleza Jaji Cecil Githua kuwa msaidizi huyo wa Bw Obado aliendesha gari umbali wa mita 300 na kulisimamisha kisha watu wengine wawili wakaingia.

Kwa mujibu wa mpasha habari aliyeripoti tukio hilo kwa Bw Okoti, watu walioingia kwenye gari hilo walitisha kumuua kwani alikuwa anachunguza kisa cha madai ya Bw Obado kumpachika mimba msichana wa chuo.

Kwa kuhofia kuuawa, mpasha habari huyo ambaye ni shahidi anayelindwa na Serikali na jina lake halipaswi kutambuliwa, aliruka kutoka kwenye gari walimobebwa na Sharon, lilipokuwa likienda kwa kasi.

Jaji Githua anayesikiliza kesi ya mauaji inayomkabili Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Bw Michael Oyamo na aliyekuwa katibu wa kaunti, Bw Casper Obiero alifahamishwa kuwa mpasha habari huyo alipata majeraha miguuni na mikononi.

Konstebo Okoti anayehudumu katika kituo cha Polisi cha Mawengo, Kaunti ya Homa Bay alisema mlalamishi huyo alifika katika kituo cha Polisi cha Kendel mwendo wa saa tatu usiku wa Septemba 3, 2018.

“Mheshimiwa, gari aina ya Probox nambari ya usajili KBS 532R liliegeshwa katika kituo cha polisi cha Kendel likiwa na watu wawili. Dereva alishuka na kuingia afisini mwangu,” alisema Bw Okoti.

Mahakama ilielezwa kuwa dereva huyo alisema abiria aliyekuwa amembeba alikuwa na ujumbe ambao angetaka kuuripoti.

Afisa huyo wa polisi ambaye amehudumia kikosi cha polisi miaka 38, aliambia mahakama kuwa aliandika taarifa ya ushahidi kutoka kwa mwananchi huyo.

“Mwanaume huyo aliyefika kupiga ripoti hiyo ya kutekwa nyara kwa Sharon pamoja naye alikuwa na majeraha kwenye viganja vya mikono na magoti,” Konstebo Okoti alisema.

Afisa huyo alisema mwanamume huyo aliyepiga ripoti alikuwa ameshtuka.

Alisema walikuwa na Sharon katika hoteli ya Graca iliyoko Rongo walipokuwa na msaidizi wa Bw Obado.

Wawili hao walielezwa na msaidizi huyo waabiri gari waende kwenye hoteli nyingine. Walipoabiri gari hilo lilielekea upande wa Homa Bay.

“Alipokuwa ndani ya gari hilo alitishwa kuuawa kwa kuchunguza habari za gavana huyo kumtia mimba mwanafunzi wa chuo kikuu,” mahakama ilielezwa.

Kwa kuhofia maisha yake aliruka kutoka kwa gari na kumwacha Sharon ndani ya gari hilo.

Konstebo Okoti alimpigia afisa msimamizi wa kituo cha Kendu Bay apange jinsi mwananchi huyo aliyekuwa na majeraha atakavyopelekwa hospitalini kwa kuwa alikuwa akitokwa na damu.

OCS huyo wa Kendu Bay aliweka mipango ya kumpeleka kwa matibabu.

OCS huyo alitambuliwa kuwa marehemu George Njuki Kambii.

Akihojiwa na mawakili Prof Tom Ojienda, Kioko Kilukumi na Elisha Ongoya afisa huyo wa polisi alisema alitekeleza majukumu yake alipomsaidia mwananchi huyo kupelekwa hospitalini.

Obado, Oyamo na Obiero wamekana waliwaua Sharon na mtoto wake mnamo Septemba 3, 2018.

Wako nje kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 4, 2021.

You can share this post!

Utulivu mdogo Afrika Kusini baada ya jeshi kumwagwa

Babu, 93 ashinda vijana kwa mistari, aoa mke wa umri wa...