• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Utulivu mdogo Afrika Kusini baada ya jeshi kumwagwa

Utulivu mdogo Afrika Kusini baada ya jeshi kumwagwa

Na MASHIRIKA

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

UTULIVU mdogo Alhamisi ulianza kurejea maeneo machache nchini Afrika Kusini baada ya machafuko kushuhudiwa katika miji kadha nchini tangu serikali kuanza kutumia wanajeshi kutuliza fujo hizo.

Mnamo Jumatano jioni serikali ilitangaza kuwa itawatuma jumla ya wanajeshi 25,000 katika barabara kadhaa za miji kukabiliana na wanaoshiriki machafuko na uporaji wa mali.

Kufikia Jumatano, jioni jumla ya watu 72 walikuwa wameuawa katika ghasia hizo huku wengine zaidi ya 1,200 wakikamatwa, kulingana na takwimu rasmi kutoka kwa serikali.

Fujo hizo zililipuka wiki jana kufuatia kufungwa gerezani kwa rais wa zamani Jacob Zuma kwa kosa la kudharau mahakama. Kiongozi huyo alikaidi agizo la kumtaka afike mahakamani kuhudhuria vikao vya kusikizwa kwa kesi ya ufisadi inayomwandama.

Baada ya jumla ya wanajeshi 5,000 kutumwa katika mikao ya Gauteng na KwaZulu-Natal Jumatano, kufuatia amri ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, utulivu ulianza kushuhudiwa katika vitongoji kadhaa.

Hata hivyo, visa vya uporaji viliendelea kushuhudiwa katika jiji la Durban.

Wanahabari walishuhudia makundi ya watu wakisomba magunia ya unga na vyakula vinginevyo kutoka madukani na kuyapakia katika magari aina ya Pick-Up. Gari moja hata hivyo, liliachwa na waporaji hao baada ya kuisha mafuta.

Alhamisi vituo vya mafuta katika jiji hilo lililoko karibu na ufuo wa bahari vilikuwa vimefungwa kutokana na machafuko hayo.

Visa vya uporaji mali viliathiri shughuli za kibiashara na uchukuzi katika maeneo ya KwaZulu-Natal ambako Bw Zuma ana umaarufu mkubwa.

Alhamisi, serikali ilisema imenakili jumla ya visa 208 vya uporaji mali kote nchini Afrika Kusini.

Shirikisho la watumiaji bidhaa nchini humu ilikadiria kuwa jumla ya maduka 800 ya reja reja yaliporwa katika kipindi cha siku sita za machafuko.

Kundi la wahudumu wa magari ya uchukuzi waliokuwa wamejihami kwa rungu na bunduki walikabiliana na waporaji katika mji wa Vosloorus, kusini mashariki kwa jiji la Johannesburg.

Mfalme mpya wa jamii ya Wazulu, Misuzulu Zulu alisema ghasia hizo zimeleta “aibu kubwa” kwa watu wake.

“Ghasia hizo zinaharibu uchumi wetu, ni masikini ndio wataumia zaidi,” akaonya mfalme huyo anayeheshimika miongoni mwa jamii hiyo, japo hana mamlaka makuu.

Umoja wa Afrika (AU) nao umekashifu vikali ghasia hizo huku ukiitaka serikali ya Rais Ramaphosa kuzikomesha “haraka jinsi iwezekanavyo ili kuokoa maisha na mali.”

Mwenyekiti wa tume ya umoja huo Moussa Faki Mahamat alionya kuwa huenda ghasia hizo zikasambaa hadi katika mataifa jirani ikiwa hazitadhibitiwa.

  • Tags

You can share this post!

WASONGA: Ruwaza za kiuchumi zao Ruto, Raila ni hadaa tupu

‘Jinsi Sharon alivyosafirishwa kuuawa’