• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Jinsi waumini walioenda kesha kanisani walivyoporwa saa tisa usiku na genge lenye bunduki

Jinsi waumini walioenda kesha kanisani walivyoporwa saa tisa usiku na genge lenye bunduki

Na MERCY KOSKEI

Kile kilichoanza kama ibada katika kanisa la Joy Praise Ministry katika eneo la Heshima, Bahati, Kaunti ya Nakuru Ijumaa usiku kiliishia kwa tukio la kuogofya kwa waumini wa kanisa hilo.

Ilikuwa saa tisa asubuhi ya Jumamosi Septemba 23, 2023 wakati ambapo watu watano waliobeba silaha wakiwa kwenye pikipiki mbili walipovamia kanisa na kuamuru waumini waliokuwa wamezama kwenye maombi kulala chini.

Akihadithia tukio hilo, Stephen Mwangi, mmoja wa waumini waliokuwa kwenye kanisa hilo anasema kwamba kulikuwa na zaidi ya waumini 30 kwenye kesha hiyo.

Ijumaa usiku, karibu saa mbili hivi, waumini walikusanyika katika kanisa hilo kama kawaida kwa kesha lakini saa sita baadaye, walivamiwa na wanaume waliokuwa wamebeba bunduki na silaha butu wakati ambapo pasta alikuwa akiendelea na mahubiri.

Kanisa la Joy Praise, eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru ambalo waumini wake walivamiwa na majambazi usiku wa manane wakiwa kwenye kesha. Picha zote| Boniface Mwangi

Mwangi anaambia Taifa Leo kwamba wezi hao waliingia kanisani kupitia lango kuu ambalo lilikuwa wazi usiku mzima.

“Wanaume watatu waliokuwa na bunduki aina ya AK47 waliingia kanisani huku wawili wakibaki kwenye lango kuu kulinda,” asimulia Mwangi.

“Tulianza ibada yetu vizuri sana lakini ilipofika saa tisa tulivamiwa na majambazi. Sote tuliduwaa na kuingiwa na woga. Walituambia kama si vile hawakuwa na muda mwingi, wangetuitisha neno-siri la Mpesa. Tunashukuru Mungu hawakujeruhi yeyote, walichukua mali zetu tu za thamani,” akasema.

Anasema baada ya kuwaibia, wanaume wawili waliingia katika makazi yanayopakana na kanisa hilo na kuchukua meko ya kilo sita ambayo walitumia kupikia chai waumini ambao walikuwa waondoke saa kumi na moja alfajiri.

Mwangi anasema majambazi hao waliwaambia kwamba walikuwa kwenye misheni nyingine lakini mwenye nyumba ndiye alipiga kamsa ikabidi wawaibie ili wapate pesa waweze kutoroka.

“Walisema walihitaji sana pesa na chakula. Nilikuwa na Sh800 mfukoni ambazo walichukua. Hawakuiba vifaa vya kanisa. Walichukua paketi 25 za keki ambazo tulikuwa tule na chai ya alfajiri,” alisema.

Lucy Njeri, muumini mwingine anahadithia kwamba wakati uvamizi ulipofanyika, alikuwa analala kwenye afisi ya kanisa baada ya kulemewa na usingizi kabla arejee kwenye maombi tena.

Anasema alisikia mtafaruku ndani ya kanisa kabla ya kila kitu kunyamaza.

Anasema alishtuka wakati mtu alipomgusa kwa bega na kumwambia ampe simu aliyokuwa nayo kabla ya kumsindikiza ndani ya kanisa ambapo kila mtu alikuwa amelala kifudifudi.

“Alikuwa mwanamume mrefu, uso wake ulikuwa umefunikwa na alikuwa na bunduki. Aliniagiza nitoke nje. Nilipotoka nje niliona mwanamume mwingine ambaye pia alikuwa amebeba silaha. Hapo ndio nilibaini kwamba tumevamiwa,” akasema.

Muda mfupi baada ya kulala chini, Njeri anasema wezi hao walimwagiza kuzima taa.

Anasema walichukua simu yake kabla ya kurudi kwenye afisi na kuchukua Sh3,000 ambazo zilikuwa sadaka zilizotolewa.

Kulingana na Njeri, ilikuwa mara ya pili ya kuvamiwa na wezi baada ya jaribio la awali kufeli baada ya kupiga kamsa.

“Baada ya kulala chini, walininyanyua tena na kuniamuru nitoe neno-siri la Mpesa ya pasta wetu. Niliwaambia sikua naijua, kwamba bado nilikuwa mgeni katika kanisa hilo. Walimwambia pasta wetu kwamba hawatachukua vifaa vyovyote, hata wakatusihi tuwaombee,” ahadithia Njeri.

Nancy Wangui, ambaye amekuwa muumini wa kanisa hili kwa mwaka mmoja sasa anasema kwamba bado amepigwa na mshtuko kuhusu waliyopitia haswa kufuatia simu yake mpya kuchukuliwa.

Anasema alikuwa amekaa nyuma wakati mmoja wa majambazi hao alipomsukuma mbele. Anasema hakupiga nduru akidhani walikuwa maafisa wa polisi akisema walikuwa wamevalia mavazi rasmi ya polisi.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Bahati Nganga Mwangi anasema kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha Kiugoine na kwamba wameanzisha uchunguzi.

Aliomba mtu yeyote aliye na habari ambazo zinaweza kusaidia kunaswa kwa majambazi hao apige ripoti kwenye kituo chochote nchini akisema wameimarisha doria eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Mahasla sasa kukutana na mkono mrefu wa serikali katika...

Mkono wa vidume wa kisiasa kwenye masaibu ya Kawira

T L