• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Jumwa na wengine 6 wataka kesi ya ufisadi dhidi yao isikilizwe upya

Jumwa na wengine 6 wataka kesi ya ufisadi dhidi yao isikilizwe upya

Na PHILIP MUYANGA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, na watu wengine sita wanaokabiliwa na mashtaka ya kushiriki ufisadi, sasa wanataka kesi yao isikilizwe upya baada ya kuhamishwa kwa hakimu aliyeishughulikia.

Kupitia wakili wao Danstan Omari, mbunge huyo na washtakiwa wenzake wamemweleza Hakimu Mkuu wa Mombasa Martha Mutuku kuwa, wanataka kesi hiyo ianze upya ili kuipa korti nafasi ya kuwatathmini mashahidi.

“Tunaomba mahakama kesi hii ianze upya ili korti iwachunguze wanaotoa ushahidi na uhalali wa ushahidi huo. Huo ndio msimamo wa upande wa utetezi,” akasema Bw Omari.

Hata hivyo, viongozi wa mashtaka Henry Kinyanjui na Alex Akula walipinga wakisema kuwa, amri ilitolewa kwamba kesi hiyo iendelee kutoka pahali ilipoachiwa na hakimu wa awali.

Walieleza korti kwamba mashahidi watatu tayari wametoa ushahidi wao na wanalenga kuwaita wengine 17 kuipa nguvu kesi yao.

Katiba inampa mshtakiwa haki ya kutaka kesi yake isikizwe upya iwapo hakimu aliyekuwa akisimamia mwanzoni atahamishwa hadi korti nyingine.

Pia mshtakiwa yupo huru kuamua kesi hiyo iendelee chini ya hakimu mpya.Bi Mutuku alizitaka pande zote mbili ziwasilishe hoja zao azitathmini ndipo atoe uamuzi.

Mbunge huyo ameshtakiwa kwa madai ya kuilaghai serikali kupitia Hazina ya Kitaifa ya Ustawi wa Maneobunge (CDF) ya Malindi jumla ya Sh19 milioni, zilizolipwa kampuni ya Multiserve iliyopewa kandarasi na Bi Jumwa.

Mwakilishi huyo alishtakiwa pamoja na Bw Wachu Omar, Kennedy Otieno, Bernard Riba, Sophia Saidi, Margaret Kalume, Robert Katana na wanakandarasi wa kampuni hiyo ya Multiserve.

Wote wamekana mashtaka huku kesi ikiratibiwa kutajwa Janauri 17, ambapo tarehe ya kusikizwa itawekwa upya.

You can share this post!

Macho kwa Kamworor akivizia rekodi ya dunia ya Eliud...

Wanaotapeli kwa jina la mkewe Ruto wasakwa na polisi

T L