• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kamati yaundwa kuangazia kilio cha wafanyakazi wa Malindi Water

Kamati yaundwa kuangazia kilio cha wafanyakazi wa Malindi Water

NA ALEX KALAMA 

SERIKALI ya kaunti ya Kilifi kupitia afisi ya gavana Gideon Mung’aro, imeunda kamati itakayochunguza malalamiko ya wafanyakazi wa kampuni ya maji ya Malindi Water (MAWASCO) walioandamana mnamo Alhamisi asubuhi.

Shughuli za usambazaji maji zilitatizika pakubwa.

Maswala ambayo wafanyakazi hao wamekuwa wakitaka yaangaziwe ni malipo wakitaka mishahara iongezwe, na kurekebishwa kwa makato kama ya Hazina ya Mafao ya Uzeeni (NSSF) na fedha nyingine za kuweka akiba ambazo licha ya kukatwa tangu 2018 haijulikani zinakoelekezwa.

Akizungumza na wanahabari katika makazi yake, Gavana Mung’aro alieleza kuwa baada ya ripoti ya kamati hiyo kufikishwa mbele yake, afisi yake itachukua hatua mwafaka kutatua matatizo ya wafanyakazi hao.

“Kwa hiyo hatua ambayo tunasema ya kwanza ni kuanzisha jopo maalum ambalo litaleta ripoti kwangu baada ya wiki mbili kuhusu uchunguzi na maswala yale yote ambayo wafanyaakazi wa kampuni ya MAWASCO wamelalamikia,” alisema Bw Mung’aro.

Aidha alitishia kuitimua bodi hiyo iwapo kutapatikana na makosa.

“Pia bodi ya wakurugenzi wanaongoza kampuni hiyo ya maji ninashauri wateue mkaguzi wa hesabu ili kufanya ukaguzi wa kina kwenye kampuni hiyo ya Malindi Water. Vilevile nimeagiza hiyo bodi ikamilishe kumteua mkurugenzi mkuu mpya atayeongoza na kuiendesha kampuni hiyo,” alisema Bw Mung’aro.

Kulingana na bodi hiyo, kampuni ya MAWASCO ilipoteza mamilioni ya pesa kutokana na shughuli za kampuni hiyo kukwama siku nzima mnamo Alhamisi baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kugoma.

Hatua ya Mung’aro kuagiza bodi inayoongoza kampuni hiyo kukamilisha mchakato wa kumteua mkurugenzi mkuu mpya imejiri miezi michache tu baada ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Gerald Mwambire kutimuliwa na kisha nafasi yake kupewa kaka yake naibu gavana wa Kilifi ambaye kwa sasa anashikilia nafasi hiyo kama kaimu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ yaahirishwa

DOMO: Yamewakuta basi iwe funzo

T L