• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
DOMO: Yamewakuta basi iwe funzo

DOMO: Yamewakuta basi iwe funzo

NA MWANAMIPASHO

ISHU ya Stivo Simple Boy na The Sailors imeniacha nikiwasikitikia sana.

Wote wamejiletea msiba wa kujitakia na sasa kimawaramba. Stivo juzi amejitokeza na kusema anapitia kipindi kigumu sana baada ya menejimenti yake Men In Business (MIB) kumtumia vibaya.

Mara tu baada ya kauli hiyo, MIB ilitoa taarifa ikisema imevunja mkataba na Stivo. Hapa nilipo nimejaribu kuangalia alichofaidi Stivo au MIB ilimfaidi vipi, na kwa kweli nimeshindwa kuona la mno.

Nimebaki kumlaumu Stivo kwa kuwa na akili fupi. Inawezekana aliwaamini sana, au hakutegemea yatamfika yaliyomfika ila alistahili kuwa makini sana.

Japo ya kujipatia umaarufu Stivo hajaweza kujisaidia. Kuna kipindi alikuwa analamba dili za ubalozi na matangazo ya biashara, nashangaa hadi sasa hazikumsaidia. Kwa nini namlaumu? Baada ya kupata umaarufu Stivo kama vile alijisahau na kuiachia MIB mamlaka yote ya kuendesha shughuli. Sijui kwa nini aliwaamini sana.

Angalau kabla ya kusaini nao mkataba, Stivo alichostahili kufanya ni kuipiga msasa MIB kuhusu utendaji wao. Je, kuna msanii mwingine wamewahi kusimamia? Na kama ndio msanii huyo yuko wapi na mambo yake yanamwendeaje?

Kwa busara zangu MIB haijawahi kumsimamia mtu yeyote isipokuwa Stivo. Sasa basi kwa nini Stivo alishindwa kuliona hili? Wamemtumia, wakakulia sifa zake na baada ya kugundua hana tena tija wala havutii dili zaidi, wamemtoka sasa Stivo kageuka ombaomba mitandaoni.

Sailors ni wengine vile vile. Kipindi wanaanza, alitokea mdau wa burudani nchini Mwalimu Rachel aliyeamua kuwashika mkono. Sio kwamba Rachel amewahi kumsimamia msanii ila kubobea kwake kwenye tasnia ya burudani kulimtosheleza kuelewa masuala ya namna tasnia yetu ilivyo.

Chini ya Rachel, Sailors walionekana kuwa na ndoto ya kufanikisha. Ngoma zao zikasikika na kila leo, walizungumziwa. Ghafla yakazuka madai kutoka kwao kwamba Mwalimu Rachel kawaosha hela. Haya majungu yakaishia kumkatisha tamaa Rachel akaachana nao.

Rachel kwa upande wake anadai madogo waliingiwa na tamaa baada ya kuona mafanikio yao na kuanza kumwona kama kupe anayewafaidi. Basi akaachana nao na ukawa ndio mwisho wa Sailors.

Juzi nimemsikia kinara wa Sailors Miracle Baby akidai chanzo cha kusambaratika kwa kundi kilisababishwa na makateli fulani Wakenya waishio Marekani. Sikutaka kumsikia sana dogo maana niliona kama vile hajielewi. Si ni yeye tu aliyewahi kumlaumu Mwalimu Rachel, leo sasa analaumu makateli. Pole kwao. Kimeramba ila natumai itakuwa funzo, muziki unahitaji akili na hekima.

  • Tags

You can share this post!

Kamati yaundwa kuangazia kilio cha wafanyakazi wa Malindi...

Kijiji cha Busho chapata kituo cha kidijitali

T L