• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ yaahirishwa

Kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ yaahirishwa

NA TITUS OMINDE

KUSIKILIZWA kwa kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa mashoga na wasagaji (LGBTQ) Edwin Kipruto almaarufu Chiloba kuliahirishwa huku upande wa mashtaka ukiwa tayari na mashahidi zaidi ya 20 kutoa ushahidi dhidi ya mshukiwa mkuu wa mauaji hayo ya kinyama.

Haya yamebainika mnamo Ijumaa baada ya Jaji Reuben Nyakundi wa mahakama kuu ya Eldoret ambaye amekuwa akisikiliza kesi hiyo kukosa kufika mahakamani baada ya kupata msiba.

Akiwafahamisha mashahidi hao kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili wa serikali Mark Mugun amesema miongoni mwa mashahidi wakuu kuna wanafunzi watatu wa chuo kikuu, mlinzi wa jengo alimokuwa marehemu, na dereva wa teksi.

Wanatarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa Jacktone Odhiambo.

Marehemu Chiloba alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Eldoret, akisomea shahada ya msawala ya mitindo na ubunifu.

Bw Odhiambo ambaye anazuiliwa katika gereza la Eldoret GK tangu kukamatwa kwake, amekana kumuua Chiloba kati ya Desemba 31, 2022 na Januari 3, 2023.

Hati ya mashtaka inaonyesha kuwa alitenda kosa hilo katika ghorofa ya Noble Breeze eneo la Chebisas katika kaunti ndogo ya Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Mara ya mwisho alipokuwa kortini, Odhiambo, alipoulizwa na Jaji kueleza ni kwa nini alikuwa kizimbani, alisema: “Niko hapa kwa sababu mimi ni mshukiwa wa mauaji ya Edwin Chiloba.”

Aidha alimweleza jaji kuwa anafahamu mashtaka yanayomkabili lakini akaharakisha kuongeza kuwa hakumuua Chiloba jinsi inavyodaiwa.

Upande wa mashtaka unaongozwa na Bw Mugun huku wakili Mathai Maina akimwakilisha mshtakiwa.

Mnamo Februari, mahakama iliwaachilia washukiwa wanne miongoni mwao akiwemo mnyanyuaji uzani Dennis Litali, aliyehusishwa na mauaji ya Chiloba baada ya upande wa mashtaka kusema kuwa hauna ushahidi wa kuwashtaki baada ya kukamilika kwa siku 21 za uchunguzi.

Mwili wa mwanaharakati huyo wa LGBTQ ulipatikana kwenye sanduku la chuma kando ya barabara ya Kipkenyo-Kaptinga katika kaunti ndogo ya Kapseret katika Kaunti ya Uasin Gishu mnamo Januari 3.

Uchunguzi wa maiti ambao ulifanywa kwenye mwili wa marehemu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) ulibaini kuwa marehemu aliaga dunia kwa kukosa hewa safi ya oksijeni.

Kifo chake kilivutia jamii ya kimataifa iliyoangaza sauti kulaani unyama huo.

Kesi hiyo sasa itasikilizwa Julai 20, Agosti 3 na Agosti 4 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Ushuru wa juu wazuru mifuko ya Wakenya

Kamati yaundwa kuangazia kilio cha wafanyakazi wa Malindi...

T L