• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Kamket huru kwa bondi, azuiwa kukanyaga guu Baringo

Kamket huru kwa bondi, azuiwa kukanyaga guu Baringo

Na JOSEPH OPENDA

MAHAKAMA moja ya Nakuru Ijumaa ilimwachilia huru Mbunge wa Tiaty, William Kasait Kamket kwa dhamana ya Sh500,000.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mkuu Lilian Arika alikataa ombi lililowasilishwa na polisi kwamba, Bw Kamket azuiliwe kwa siku 14 zaidi ili wakamilishe uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomhusisha na mashambulio katika eneo la Ol Moran, Kaunti ya Laikipia.

Mbunge huyo aliyekamatwa Jumatano, alizuiliwa kwa siku mbili katika kituo cha polisi cha Kaptembwa akisubiri ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo, Bi Arika alisema hakuna sababu yenye mashiko ya kuzuiliwa kwa mshukiwa bila kufunguliwa mashtaka kortini.Hakimu huyo alieleza kuwa polisi hawazuiliwi kuendelea na uchunguzi wao hata baadhi ya kushtakiwa kwa mshukiwa.

“Sijaridhika kwamba sababu za kuendelea kuzuiliwa mshukiwa na kumnyima dhamana. Kwa hivyo, nimekatalia mbali ombi hilo la polisi,” akasema.

Hata hivyo, hakimu huyo alitoa masharti makali ambayo Bw Kamket anafaa kuzingatia wakati wa uchunguzi.

Masharti hayo yanajumuisha kuzuiwa kufika nyumbani kwake katika eneobunge la Tiaty, kutoa matamshi yanayoweza kuchochea chuki na kusalia nyumbani kwake katika Kaunti ya Nakuru.

Katika ombi liliwasilishwa Alhamisi, polisi waliambia korti kwamba, wanamchunguza Kamket kuhusiana na madai ya mauaji, kuchochea fujo, wizi wa mifugo, wizi wa mabavu na kudharau sheria.

Kupitia wakili wa serikali Alloys Kemo, polisi walisema wana sababu za kuamini kuwa Bw Kamket alihusika katika kupanga na kushirikisha mashambulio katika kaunti ya Laikipia yaliyosababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali.

You can share this post!

Walimu 3 waliohitimu PhD wafunza katika chekechea, Gredi ya...

Kemsa lawamani tena hospitali zikikosa dawa