• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Kampuni yagundua kiwango kikubwa cha dhahabu

Kampuni yagundua kiwango kikubwa cha dhahabu

BENSON AMADALA Na DERICK LUVEGA

UCHIMBAJI wa dhahabu Magharibi mwa Kenya unatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa baada ya kampuni ya Shanta Gold ambayo imekuwa ikitafuta madini hayo eneo hilo kuripoti kuwa imepata dhahabu katika maeneo saba tofauti.

Madini hayo yanakadiriwa kuwa ya thamani ya Sh164 bilioni na yanaweza kuchimbwa kwa miaka kumi ijayo.

Kampuni ilisema ilichimba mashimo kumi na moja kati ya Machi na Aprili mwaka huu katika mradi wa Magharibi mwa Kenya uliochukua kilomita 1,162 mraba eneo la Isulu, Liranda ambako ilipata dhahabu hiyo. Mashini za uchmbaji zingali katika maeneo ya Isulu na Bushiangala.

Kampuni inapanga kuongeza idadi ya mashini hadi tatu kufikia kati kati ya mwaka huu. Afisa wa kampuni hiyo alifahamisha Taifa Leo kwamba, itachukua muda wa miaka mitano kabla ya uchimbaji kuanza rasmi.

Kwenye taarifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Eric Zurrin alisema, upatikanaji wa dhahabu hiyo unaonyesha kuwa kuna dhahabu ya hali ya juu.

“Kwa sasa, uchimbaji umefichua kwamba kuna maeneo yaliyo na dhahabu ya gredi ya hali ya juu na tunatarajia kutoa maelezo zaidi tunapoendelea,” alisema.

Kampuni ilisema inatarajia kukamilisha utafutaji wa madini hayo eneo la Magharibi mwa Kenya kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Bw Evans Masachi, mkurugenzi wa Uzalishaji wa Madini wa Kaunti, alisema atawasilisha ripoti kwa serikali ya kitaifa ili hatua zaidi zichukuliwe.

“Kwa sasa tumekuwa tukizuru eneo la Bushangala ambapo tunafanya mazungumzo na wachimbaji wadogo wa dhahabu. Kisha tutawasilisha ripoti kwa serikali kuu,” akasema Bw Masachi.

You can share this post!

Wito serikali itoe sodo bila malipo

IEBC yalaumu polisi kwa vurugu za chaguzi ndogo