• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Karen Nyamu – Watu wanapendekeza Kituo cha Polisi Kasarani kigeuzwe kuwa soko

Karen Nyamu – Watu wanapendekeza Kituo cha Polisi Kasarani kigeuzwe kuwa soko

NA SAMMY WAWERU

SENETA maalum Karen Nyamu ameitaka serikali kuchunguza Kituo cha Polisi cha Kasarani kufuatia malalamishi ya umma kuhusu utepetevu wa utendakazi.

Himizo hilo limetolewa kufuatia mauaji ya kinyama ya kijana Geoffrey Mwathi, Bi Karen akisema yamefichua mengi kuhusu utendakazi mbovu wa kituo hicho.

Kulingana na mwanasiasa huyo wa chama cha UDA, askari wa kituo hicho waliohusika katika uchunguzi wa awali wa Geoffrey maarufu kama Jeff walishirikiana na washukiwa wa mauaji kuficha maovu.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 ni mpwa wa muimbaji wa nyimbo za Mugithi Bw Samuel Muchoki almaarufu Samidoh, na alifariki katika nyumba ya mcheza santuri Fatxo.

Fatxo ambaye majina yake kamili ni Lawrence Njuguna Waguru, anahusishwa na mauaji hayo kama mshukiwa mkuu.

“Nimekuwa nikifuatilia kesi ya Jeff kutafuta haki, ikiwemo kuzuru Kituo cha Polisi cha Kasarani. Ninathibitisha kwamba maafisa wa polisi wa kituo hicho waliotwikwa jukumu kufanya uchunguzi walihusika kuficha ukweli usibainike,” Karen akadai.

Alitoa madai hayo mnamo Jumamosi akizungumza katika Kaunti ya Kirinyaga katika hafla iliyohudhuriwa na Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua katika Shule ya Upili ya Kianyaga.

Seneta huyo aidha alitumia jukwaa hilo kushawishi serikali ichunguze kituo cha Kasarani, akilalamika kuwa wengi wa wanaowasilisha kesi humo ni vigumu kupata haki.

“Wahusika wa mauaji ya Jeff watakapofikishwa kortini, tunakuomba (Naibu wa Rais Gachagua) utusaidie kusafisha kituo hicho,” akasema.

Karen alidokeza kwamba kupitia kurasa zake za mitandao, wananchi wanapendekeza kifungwe na nafasi yake igeuzwe kuwa soko.

“Hapo hakuna kituo. Isitoshe, kupitia jumbe ninazopokea kwenye Facebook, watu wanapendekeza kifungwe na nafasi yake igeuzwe kuwa soko.”

Kesi ya Jeff imetwaliwa na kitengo maalum kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI), kinachoshughulikia masuala ya mauaji.

Kijana huyo aliuawa mnamo Februari 22.

  • Tags

You can share this post!

Jennifer Kananu Mbogori ni mwasisi wa kampuni ya...

Mama yake Ruto arai pawepo amani nchini

T L