• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 2:11 PM
Kaunti zahimizwa kukumbatia mpango wa kufikisha ushauri wa shughuli bora za kilimo mashambani, VBA

Kaunti zahimizwa kukumbatia mpango wa kufikisha ushauri wa shughuli bora za kilimo mashambani, VBA

Na SAMMY WAWERU

Zaidi ya wakulima 200,000 Kaunti ya Kiambu wamenufaika kupitia mpango wa utoaji ushauri kuimarisha shughuli za kilimo, maarufu kama Village Based Advisory (VBA).

Mpango huo unajumuisha wakulima wanaoendesha kilimo, wanapata mafunzo maalum ili kuyatoa kwa wenzao.

Aidha, wanafunza mbinu za kisasa; matumizi ya pembejeo (fatalaiza, mbegu na dawa) zilizoimarishwa kuboresha kilimo.

Kulingana na Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro, lengo la mpango huo unaofadhiliwa na serikali ya kaunti na Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), unapania kupiga jeki sekta ya kilimo.

Ulizinduliwa Kiambu mwaka wa 2018, na wakulima wamefaidi kupitia usambazaji wa fatalaiza, mbegu na dawa bora, katika mchakato mzima kuongeza kiwango cha mazao.

Waliofaidi kufikia sasa ni wakuzaji wa mahindi na maharagwe, Gavana Nyoro akisema hivi karibuni mradi huo utaanza kujumuisha wakulima wa viazi, alizeti (sunflower), kati ya mimea mingineyo.

“Tunachofanya ni kuafikia na kutekeleza ajenda kuu ya AGRA, kuhakikisha taifa na Bara la Afrika kwa jumla lina chakula cha kutosha na salama,” akasema Dkt Nyoro.

Tangu mpango huo uzinduliwe Kiambu, zaidi ya maafisa 1,000 wa VBA wamesajiliwa, kuelimishwa na kupata mafunzo kuhusu kilimo bora na faafu.

Licha ya kuwa wanatekeleza hayo bila malipo, kaunti inawafadhili kwa pembejeo, wanajukumika kufikia wakulima wengine.

Mwanzo, wanatumia fatalaiza, mbegu na dawa katika mashamba yao, ili wenzao kujifunza mengi.

“Tulianza kwa maafisa 50 wa VBA na kufikia sasa tuna zaidi ya 1,000. Tunatambua wakulima tunaofanya kazi nao, wanafanyia jaribio pembejeo na teknolojia tunayohimiza ili waeneze ujumbe kwa wenzao,” Nyoro akafafanua.

Akisifia mfango huo, Gavana alisema wakulima wamekadiria ongezeko la mazao na ubora.

“Pembejeo na teknolojia tuliyokumbatia, wakulima wanakiri kuna ongezeko la mazao. Tumeshuhudia baadhi wakivuna mazao mara dufu, mfano ongezeko la mahindi kutoka gunia moja kila ekari hadi karibu magunia kumi,” Bw Nyoro akaelezea.

Alidokeza kwamba mwaka huu wa 2021, Kaunti ya Kiambu imetumia Sh75 milioni kufanikisha mpango huo, akisema kufikia 2022 inapanga kuutengea kati ya Sh100 milioni na Sh150 milioni.

“Tumeshuhudia VBA ina manufaa chungu nzima kwa wakulima. Tunahimiza kaunti nyinginezo nchini ziige. Ninaendelea kufanya mazungumzo na magavana kupitia Baraza la Magavana , CoG,” akasema gavana huyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika CoG kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Katika ziara yake Kiambu kutathmini utekelezaji wa VBA, mwenyekiti wa AGRA, Hailemariam Desalegn alisema usalama na namna ya kuimarisha utoshelevu wa chakula Barani Afrika, ndiyo masuala yatakayoangaziwa kikamilifu endapo sekta ya kilimo itapewa kipaumbele kwenye mgao wa bajeti.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn (kushoto) na ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa AGRA na Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro wakati wa ziara katika shamba la mmoja wa wakulima, ambaye ni afisa wa VBA, eneo la Ikinu, Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

“Kuna haja ya kuwa na kuleta uongozi unaothamini shughuli za kilimo, kupitia mgao wa bajeti ya serikali kwa kutengea sekta hii fedha za kutosha na kuimarisha soko,” akahimiza waziri huyo mkuu wa zamani Ethiopia.

Sekta ya kilimo hata hivyo imegatuliwa, kupitia Katiba ya sasa na ambayo ilizinduliwa 2010.

Desalegn vile vile alishauri wakulima kukumbatia mbinu bora za kilimo, ili kuboresha mazao.

“Kwa kufanya hivyo baadhi ya nchi ambazo zimeshuhudia upungufu wa chakula hasa kipindi hiki cha Covid-19 kupitia amri ya mara kwa mara maeneo mengi kufungwa, kuzuia maenezi, utaangaziwa. Isitoshe, wakulima wanapaswa kupigwa jeki kupata pembejeo bora na pia kuhamasishwa mbinu faafu za kilimo, wasirejelee zile za kitambo,” akafafanua.

AGRA hulenga kuinua wakulima wadogowadogo na wale wa kadri kuimarika kimaisha, kuondoa njaa na umaskini.

“Mpango huu unaendelea kuzaa matunda, na tunaiomba serikali ya kaunti angalau kutupa mshahara ili tuweze kufikia wakulima,” akasema Hannah Mbugua, mmoja wa maafisa wa VBA.

You can share this post!

NDONDI: Nahodha Nick ‘Commander’ Okoth kuongoza...

Kiungo Toni Kroos wa Ujerumani aangika daluga zake kwenye...