• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Kaunti zahimizwa kukumbatia sheria ya kudhibiti upakiaji wa viazi

Kaunti zahimizwa kukumbatia sheria ya kudhibiti upakiaji wa viazi

Na SAMMY WAWERU

KAUNTI ambazo hazijakumbatia sheria ya kudhibiti upakiaji wa viazi mbatata zimehimizwa kuitekeleza.

Katibu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Samaki Prof Hamadi Boga. Pichaamesema sheria na mikakati ya upakiaji wa viazi ilizinduliwa ili kulinda wakulima.

Amesema kwa muda mrefu, wakuzaji wa viazi nchini wamekuwa wakihangaishwa na mawakala kupitia upakiaji wa mazao kupita kiasi.

Viazi. Picha/ Sammy Waweru

Sheria ya kudhibiti upakiaji wa viazi, ambapo mkulima anapaswa kuuza kwa kutumia mfuko au gunia lisilozidi kilo 50, ilichapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Desemba 2019 na kuanza kutekelezwa mapema 2020.

“Ninashauri kaunti ambazo huzalisha viazi na hazijaanza kutekeleza sheria za upakiaji zizikumbatie,” akashauri Prof Boga, akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, katika hafla iliyoleta pamoja wadau husika katika sekta ya viazi nchini.

“Sheria na mikakati hiyo ilizinduliwa ili kunusuru mkulima ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihangaishwa na mabroka kupitia upakiaji wa mazao kupita kiasi,” akaelezea.

Kaunti ya Nakuru na Nyandarua tayari zimekumbatia kanuni hizo, wafanyabiashara wahuni wanaozikiuka wakijipata kuandamwa na mkono wa sheria.

Aidha Katibu alisema mkulima na ambaye hubeba gharama yote ya kuzalisha viazi, atanufaika endapo washikadau wote watashirikiana kuhakikisha hakandamizwi katika soko.

“Kwa kaunti ambazo zimekumbatia sheria hizo, ninawapongeza na kuwahimiza muendelee vivyo hivyo,” Prof Boga akasema.

Viazimbatata vinaorodheshwa kama zao la pili bora, lililosheheni wanga (carbohydrates), baada ya mahindi.

You can share this post!

Maelfu bado wang’ang’ana kutoroka huku hofu ikienea

Washukiwa wawili wa ugaidi wakamatwa Likoni, Mombasa