• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Kenya yapokea dozi 880,320 za chanjo aina ya Moderna

Kenya yapokea dozi 880,320 za chanjo aina ya Moderna

Na KENYA NEWS AGENCY

SERIKALI Jumatatu ilipokea msaada mwingine wa dozi 880,320 za Moderna kutoka serikali ya Amerika.

Chanjo hizo zilizopokewa na Waziri msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman zinakuja wiki mbili baada ya nchi kupokea shehena ya kwanza ya dozi 880,460 ya chanjo hiyo.

Kufikia sasa, Kenya imepokea msaada wa chanjo 5,146,780 za corona.

Dkt Aman alisema msaada huo utakuwa wa manufaa wakati huu ambapo serikali inafanya kampeni ya chanjo kwa umma.

“Tunashukuru kwa msaada ambao tumepokea kutoka kwa mashirika na wafadhili mbalimbali. Wizara ya Afya inapiga hatua katika utoaji wa chanjo kwa umma. Hivyo, nashukuru nchi ya Amerika kwa misaada yao,” akasema Dkt Aman.

Chanjo ya Moderna ndiyo ya pili kuletwa nchini tangu serikali kuanza kutoa chanjo ya AstraZeneca mnamo Machi 2021.

Wiki iliyopita, serikali ilipokea dozi 141,600 za Johnson and Johnson kutoka serikali ya Afrika Kusini.

Dkt Aman alithibitisha kuwa kufikia sasa, Wakenya 2,050,377 wamepokea dozi yao ya kwanza huku 812,151 wakipata dozi zote.

Aliwapongeza Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi kupokea chanjo.

“Kulingana na ripoti tunayopata, tuna hakika kuwa kufikia Desemba 2021, Wakenya 10 milioni watakuwa wamepokea chanjo,” akasema Dkt Aman.

Waziri msaidizi huyo aliomba Wakenya ambao hawajapokea dozi ya pili kujitokeza kufanya hivyo.

You can share this post!

Wamalwa ahimiza viongozi wa OKA wasiwe na ubinafsi

Makala ya michezo: Winga na nahodha ambaye ameongeza...