• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Kesi dhidi ya Babu Owino yakosa kuendelea

Kesi dhidi ya Babu Owino yakosa kuendelea

NA RICHARD MUNGUTI

VIONGOZI wa mashtaka wanne jana Alhamisi walikosa kufika kuendeleza kesi inayomkabili Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.

Hakuna sababu yoyote iliyotolewa na mawakili hao wa serikali ya kutofika mbele ya Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Milimani Lucas Onyina.

Wanne hao ni Joseph Riungu, Joseph Gachoka, Jacinta Nyamosi, na Victor Owiti.

Kufuatia kutofika kwao kortini, Bw Owino pamoja na mawakili Danstan Omari na Duncan Okatchi walilalamika vikali wakisema “afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma inadharau haki za washukiwa.”

Owino alilalamika kuwa alifika kortini saa mbili asubuhi jana Alhamisi na viongozi wa mashhtaka hawakufika kuendelea na kesi ambapo Afisa Mkuu wa Polisi katika kituo cha Kilelesahwa (OCS) alitakiwa pia kueleza jinsi ambavyo Calvince Okoth Otieno almaarufu Gaucho alichapwa na wahuni 30 akiwa ndani ya seli katika kituo hicho cha polisi.

Owino na Gaucho wameshtakiwa pamoja na Tom Odongo, Michael Otieno, Pascal Ouma, Kelvin Wambo na Willy Barak kwa kile kinadaiwa ni kushiriki njama za kuivuruga serikali kutokana na hali ngumu ya maisha na kupanda kwa bei za bidhaa.

Gaucho aliomba OCS wa Kileleshwa na Inspekta Kiprop aliyemtambua kuwa mmoja wa wahuni waliomshambulia akiwa seli, wafike kortini kuhojiwa.

Alipigwa usiku wa Julai 20, 2023 na kuumizwa.

Alitibiwa katika hospitali ya Mbagathi na ripoti kuwasilishwa katika mahakama.

“Twaomba maafisa hawa wawili wakuu wa polisi waagizwe wafike kortini kujibu maswali kuhusu wahuni waliomshambulia Gaucho,” Omari alisisitiza.

Kesi itatajwa Septemba 5, 2023, kwa maagizo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Hatutaki Eldoret kuwa jiji, tunataka pesa zetu, waathiriwa...

Wanaokataa kulipa mkopo wa Hasla kujuta

T L