• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Khalwale: Mwalimu mkuu wa Mukumu akome kuingilia vyombo vya habari

Khalwale: Mwalimu mkuu wa Mukumu akome kuingilia vyombo vya habari

NA WANGU KANURI

SENETA wa Kakamega Boni Khalwale amemsuta mwalimu mkuu wa Shule ya Wasichana ya Sacred Hearts Mukumu, Fridah Ndolo, kwa matamshi yake kuhusu vyombo vya habari.

Kulingana na Bw Khalwale, matamshi ya mwalimu huyo yanaashiria kuzima uhuru wa vyombo vya habari vilivyofichua hali mbaya ya shule hiyo iliyosababisha vifo vya wanafunzi wawili.

Bi Ndolo kwa ujumbe wake kwa wazazi wa wanafunzi katika shule hiyo, alilaumu vyombo vya habari kwa kuangazia kufungwa kwa shule hiyo.

Kando na visa vya wanafunzi wawili kuaga, wengine 246 wanaendelea kupata matibabu baada ya kuugua.

Wanafunzi hao walikula chakula kibovu na kunywa maji machafu hali iliyowasababishia matatizo ya kuendesha, kutapika na kujihisi kichefuchefu.

Shule ya Wasichana ya Sacred Hearts Mukumu. PICHA / MAKTBA

Mwalimu huyo alisema, “Hii ni kuwajulisha kuwa baada ya mazungumzo ya kina na wakuu kutoka Wizara ya Elimu na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), watoto watachukua muda kukaa nyumbani ili wajihisi vyema kutokana na mazingira yenye madhara kutoka kwa vyombo vya habari.”

Seneta Khalwale alichukizwa na matamshi yake, hasa kuingilia vyombo vya habari kwa kuangazia hali mbovu ya shule hiyo na kufungwa kwake.

“Ujumbe wake kwa wazazi kuhusiana na kufungwa kwa shule ya Mukumu, mwalimu mkuu huyo hajali kuingilia uhuru wa vyombo vya habari,” alisema seneta.

Jumatatu wiki hii, Dkt Khalwale alizuru shule hiyo pamoja na Mwakilishi wa Kike kutoka Kaunti ya Kakamega Bi Elsie Muanda huku akiomba kuwa usimamizi wa shule hiyo ubadilishwe.

Maafisa kutoka Wizara ya Afya walikusanya sampuli kutoka shule hiyo wiki jana na kuzituma kwa maabara ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiafya Nchini (Kemri), lakini matokeo hayajawekwa wazi.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume auawa kinyama akitoka kilabuni

Mabaharia wanyimwa raha ya kujivinjari majuu

T L