• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Kibicho: Tutaweka kamera za siri Gikomba kudhibiti mikasa ya moto

Kibicho: Tutaweka kamera za siri Gikomba kudhibiti mikasa ya moto

Na SAMMY WAWERU

KATIBU katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho amesema serikali inalenga kupata suluhu ya kudumu kudhibiti mikasa ya moto inayoshuhudiwa mara kwa mara katika soko maarufu la Gikomba, jijini Nairobi.

Dkt Kibicho amesema baada ya kusaidia waathiriwa wanaokadiria hasara ya kupoteza mali kufuatia moto uliozuka usiku wa kuamkia Ijumaa, serikali itaweka kamera za siri Gikomba ili kubaini wanaohangaisha wafanyabiashara.

“Baada ya kuwasaidia, tutaweka kamera za siri kila mahali Gikomba zitakazokuwa zikinasa matukio saa zote,” Dkt Kibicho akasema, baada ya kufanya ziara katika soko hilo maarufu kwa bidhaa za bei nafuu, hasa nguo za mitumba.

Eneo la Molo Line, Ghorofani na ambalo ni tajika kwa mavazi ya wanawake ndilo liliathirika kutokana na mkasa huo wa moto.

Kufuatia ziara ya Katibu Kibicho, aliahidi wafanyabiashara wa Gikomba kwamba watajengewa masoko ya kudumu.

“Tayari soko moja limekamilika, litasitiri wafanyabiashara 1, 000. Tunajenga la pili,” akasema.

Dkt Karanja alisema kuwa serikali ya kitaifa inashirikiana kwa karibu na Shirika la Kuimarisha Huduma za Jiji la Nairobi, ndilo NMS kuchimba visima Gikomba, ili wafanyabiashara kupata maji.

Mikasa ya moto Gikomba si migeni, Juni 2020 wafanyabiashara katika soko hilo wakikadiria hasara nyingine ya kupoteza bidhaa.

Idara ya polisi inaendeleza uchunguzi kubaini kiini cha moto wa Ijumaa. Moto huo uliendelea kuteketeza bidhaa za mitumba kwa saa kadhaa kabla ya maafisa wa zima moto kutoka Halmashauri ya Huduma Nairobi (NMS) kuuzima hatimaye saa za alfajiri.

“Moto huo ulianza saa kadhaa baada ya usiku wa manane wakati wengi wetu tukiwa tayari tumerejea nyumbani, hivyo hatukupata nafasi ya kuokoa bidhaa zetu,” alisema mfanyabiashara katika soko hilo aliyechelea kutajwa.

Maswali yameibuka sasa kuhusiana na visa vya moto katika Soko la Gikomba huku wengi wakilaumu serikali kwa kukosa kuvikomesha.

“Tumezoa visa hivi, ni kama kawaida kila mwaka. Hata baada ya wanasiasa kuahidi kila mara vinapotokea kwamba watashughulikia kero hili mambo ni yale yale,” alisema mfanyabiashara kwa jina Kevin Njung’e.

Hata hivyo, baadhi yao wanakisia kwamba visa hivyo vinatekelezwa na wanyakuzi wa ardhi wanaomezea mate kipande cha ardhi chenye takriban ekari 30 ambapo Soko la Gikomba limejengwa.

“Mbona serikali isiwahamishe wafanyabiashara hao kwa njia ya amani ikiwa wanataka kunyakua ekari 30 za Gikomba badala ya kuvuruga juhudi zao. Ama wawajengee soko kama vile Muthurwa au soko lingine lolote la kisasa ambapo wafanyabiashara wanaweza kuwa na amani wakiaca bidhaa zao,” alihoji Kevin Mkandi, mkazi Nairobi.

Visa vya moto kuteketeza Gikomba kila mwaka vimekuwa kero kuu kwa wafanyabiashara na Wakenya kwa jumla huku ahadi za viongozi na wanasiasa kuhusu kukomesha jinamizi hilo zikisalia maneno matupu.

Kisa cha hivi punde kilijiri miezi kadhaa tu baada ya moto uliowasababishia wafanyabiashara hasara ya mamilioni mnamo Februari mwaka jana.

Zaidi ya vibanda 2,000 viliteketezwa kabisa kufuatia moto uliozuka mnamo Aprili 2019. Mwaka wa 2018 huenda ndio likuwa mbaya zaidi kwa wafanyabiashara katika Soko la Gikomba kiasi cha kumfanya Rais Uhuru Kenyatta kuitisha uchunguzi kuhusu visa hivyo.

You can share this post!

Museveni afokea Raila

Shahbal ‘avuka kisiki’ katika urithi wa Joho