• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kilio cha wazee wa MauMau Kirinyaga

Kilio cha wazee wa MauMau Kirinyaga

Na SAMMY WAWERU

KWA zaidi ya miaka 58 Mzee Boniface Ngacha amekuwa akiishi katika kipande cha shamba alichorithi kutoka kwa wazazi wake.

Bw Ngacha ni mmoja wa majasusi wa MauMau, waliotumika kupasha ujumbe vuguvugu hilo la vita vya kukomboa Kenya, kuhusu mienendo ya serikali ya Muingereza.Vita vya MauMau vilitekelezwa kati ya mwaka wa 1951 – 1957, na Juni 1, 1993 Kenya ikapata uhuru wa kujitawala.

“Jukumu letu lilikuwa kufahamisha majenerali wa MauMau waliokuwa msituni kuhusu mienendo ya askari wa mkoloni,” Ngacha anasema. Askari hao walijumuisha Wazungu, Waafrika na walinzi. Mbali na kupasha ujumbe wa mienendo yao, majasusi hao pia walitumika kuwapelekea vyakula, maji, vileo, tumbaku, sigara, silaha na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Aidha, vita vya MauMau vilitekelezwa eneo la Mlima Kenya, majukumu ya Mzee Ngacha na wenzake yakiwatia katika njiapanda na pia kuhatarisha maisha yao.Baadhi ya wapiganaji wa MauMau waliuawa kinyama mikononi mwa wakoloni dhalimu.

Licha ya Ngacha kuhatarisha maisha yake, anasema kufikia sasa serikali haijamtambua, angaa hata kumtunuku kipande cha ardhi, kutokana na jitihada zake za uzalendo.

Mzee Ngacha, na ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kang’ondu, Kaunti ya Kirinyaga, anaishi eneo la miinuko, akisema kwa shujaa kama yeye aliyesaidia kupigania uhuru wa Kenya anapaswa kuwa katika ardhi ya kuridhisha.

Picha/ Sammy Waweru.
Mzee Njogu Wameru, mkazi wa Kiangai, Ndia, Kaunti ya Kirinyaga, jasusi wa MauMau akisimulia jinsi vita vya kukomboa Kenya vilikuwa.

“Ukitazama shamba langu, ni eneo ambalo mmomonyoko wa ardhi ukijiri udongo husombwa,” anaelezea.Sawa na majasusi wengine, mhasiriwa huyu anasema anateseka umri wake ukizidi kusonga.“Tunaendelea kuteseka. Miaka inasonga na hatujui serikali itarejesha mkono lini?” ataka kujua.

Bw Ngacha hukuza kahawa, majanichai, ndizi na mboga, maumbile ya shamba lake yakimzuia kuboresha shughuli hizo za kilimo.

Kwa Mzee Njogu Wameru, jasusi mwingine, ni kumbukumbu za bidii alizotia, kuzingirwa kwa vijiji kupitia mahandaki yenye kimo cha urefu wa futi 12 yaliyochimbwa kuzuia adui kuingia, panga, mikuki na bunduki walizotumia, yote yakikolea bongoni.

“Mahandaki yaliyochimbwa yalisaidia kuzuia askari wa Mbeberu kufikia vijiji…Ni katika juhudi za kupigania uhuru wa kujitawala nilipoteza binamu yangu, aliyeuawa kinyama,” Wameru anamuomboleza.

Mhasiriwa huyu ambaye ni mkazi wa eneo la Kiangai, Ndia, Kaunti ya Kirinyaga anasema shamba analolima kahawa na majanichai ni mgao kutoka kwa mzazi wake, akilalamikia hatua ya wazee wa kijiji, machifu na wawakilishi wa serikali eneo la Kirinyaga, Kenya ilipopata uhuru kujinyakulia vipande vya ardhi na kusahau mashujaa wa MauMau.

Malalamishi ya wawili hao si tofauti na ya Mzee James Njogu Getumbo, mkazi wa kijiji cha Gathondia, Kaunti ya Kirinyaga.“Hatujakataa hata kipate cha ardhi chenye ukubwa wa ekari mbili, angaa tupanguse machozi na damu tuliyomwaga, na dhuluma tulizopitia,” Njogu anasema, mtazamo unaowiana na wazee wenza.

Mzee Njogu ni mwanachama wa vuguvugu la MauMau War Veteran Association, linalojumuisha mashujaa wa kukomboa Kenya na ambalo limekuwa likishinikiza serikali kuwatambua.

Kimsingi, kauli ya pamoja inayojitokeza kupitia mashujaa tuliozungumza nao, ni serikali kuendelea kuwapuuza, matunda ya jitihada zao yakichumwa na wale ambao hawakupitia dhuluma na unyama wa Mbeberu.

Licha ya serikali kutengea waliokula chumvi mgao wa Sh2, 000 kila mmoja kila mwezi, wanasema kupata pesa hizo imekuwa kibarua, na wengine huishia kusubiri zaidi ya miezi sita, baadhi wakidai hawajawahi kuzipata.

Awali, wakili Paul Muite alijituma kuwakilisha wanachama wa MauMau, hususan waliojeruhiwa na pia wajane wa waliofariki kupata fidia kutoka kwa serikali ya Uingereza.Mchakato huo wa kutafuta haki, unaendelea kufifia, wengi wa waathiriwa wakifariki bila kufurahia matunda ya bidii zao.

Picha/ Sammy Waweru.
Mzee James Njogu Getumbo, nyumbani kwake katika kijiji cha Gathondia, Kaunti ya Kirinyaga akisimulia alivyoshiriki vita vya MauMau

 

You can share this post!

ODM yaomboleza

MAMA ashambuliwa na wanawe Homa Bay