• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Kilio familia 89 Kwale zikihofia kufurushwa

Kilio familia 89 Kwale zikihofia kufurushwa

Na SIAGO CECE

FAMILIA 89 katika kisiwa cha Wasini, Kaunti ya Kwale, zinahofia kufurushwa makwao, baada ya mwekezaji wa kibinafsi kuanza kupima ardhi inayokisiwa kuwa na thamani ya Sh1.4 bilioni.

Familia ya Saggaf inayodai ni waathiriwa wa dhuluma za kihistoria za ardhi na ambayo miaka 17 iliyopita mahakama iliamua kuwa ardhi ya ekari 289 ni yao, sasa inazozana na familia nyingine katika kisiwa cha Wasini kutokana na masuala ambayo hayakusuluhishwa.

Taharuki ilitanda katika kisiwa hicho Jumamosi wakati maafisa wa usalama na idadi ya masoroveya ambao haikujulikana walipovamia kisiwa hicho alfajiri kupima ardhi.

Kulingana na wakazi, polisi waliitwa kuthibiti hali katika kisiwa hicho wakati wa kisa hicho cha saa kumi na moja alfajiri. Maafisa wa polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi kuwatawanya wakazi waliojawa na hasira.

“Kwa nini waje alfajiri iwapo kazi yao ilikuwa ni kufanya usoroveya pekee? Sote tunajua kwamba bwanyenye huyu anataka kututimua kisiwani,” alisema Mzee Salim Juma, mwenye umri wa miaka 70.

Shughuli zilikwama hadi Gavana wa Kwale Salim Mvurya alipoingilia kati kwa kuomba maafisa wa usalama kuacha zoezi hilo lililozua taharuki katika kisiwa hicho ambacho ni kivutio kikuu cha watalii.

Mzee Juma aliongeza kuwa familia nyingi zilizaliwa na kulelewa katika ardhi hiyo ambayo familia ya Saggaf inadai kumiliki. Bi Farhiya Juma, 79 alieleza hofu yake akisema kuwa hajui ataenda wapi iwapo atalazimika kutoka mahali hapo.

“Hii ni ardhi yetu. Hapa ndipo tulizika mababu wetu. Yeyote anayedai ardhi hii ni yake hana hata kibanda hapa. Kwa kuwa wako na pesa, wanafikiri wanaweza kutufurusha?” Bi Juma aliuliza. Wakazi hao sasa wametishia kuzua rabsha katika kisiwa hicho na katika hifadhi ya kitaifa ya viumbe wa baharini iwapo malalamishi yao hayatashughulikiwa.

Hata hivyo, mwakilishi wa familia hiyo, Bw Mohammed Maula Saggaf, alisema nia yao si kuwafurusha wakazi bali kukomboa zaidi ya ekari 200 ambazo zimetwaliwa na maskwota kwa miaka mingi.

“Hatutwai ardhi yote, ni sehemu inayomilikiwa na familia na hii inaweza kuthibitishwa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi(NLC). Tunayomiliki imenyakuliwa na wenye mahoteli na tunachotaka ni wakodishe au wainunue. Wakazi hawafai kuwa na hofu,” alisema.

You can share this post!

Musalia na Weta watakiwa kusahau urais na kumuunga mkono...

Abiria kutumia reli kutoka Mombasa hadi Malaba kuanzia...