• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Musalia na Weta  watakiwa kusahau urais na kumuunga mkono Raila 2022

Musalia na Weta watakiwa kusahau urais na kumuunga mkono Raila 2022

Na BRIAN OJAMAA

WANDANI wa kinara wa ODM Raila Odinga katika Kaunti ya Bungoma sasa wanataka viongozi wa Magharibi kusitisha azma yao ya kutaka kuwania urais na badala yake waunge mkono waziri mkuu huyo wa zamani.

Washirika hao wa Bw Odinga, wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM tawi la Bungoma, Bw Ali Balala Machani, wanamtaka kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuzingatia unabii uliotolewa zamani na kiongozi wa Dini ya Musambwa Elijah Masinde Wa Nameme.

Nabii Masinde alitabiri kuwa uongozi wa nchi hii utawafikia Waluhya kupitia Ziwani, yaani jamii ya Waluo. Kwa mujibu wa Masinde, jamii ya Waluhya itapata urais baada ya mtu wa jamii ya Waluo kuongoza nchi.

Masinde alitabiri hayo wakati makamu wa rais wa zamani Mzee Jaramogi Oginga Odinga, Michael Kijana Wamalwa na mwanasiasa Masinde Muliro, walikuwa wakipigania ukombozi wa pili baada ya wakoloni kuondoka.Masinde aliaga dunia mnamo 1987 akiwa na umri wa miaka 75.

Viongozi hao walitoa wito huo Jumamosi walipotoa msaada wa vifaa vya ujenzi vitakavyotumika kukarabati kaburi la nabii Masinde ambalo kwa sasa limechakaa.

Vifaa hivyo vilitolewa na Bw Odinga.Bw Balala ambaye pia ni diwani wa Maraka, eneobunge la Webuye Mashariki, alisema kuwa unabii wa Masinde unaelekea kutimia na mtu kutoka jamii ya Waluhya atakuwa rais baada ya Bw Odinga ambaye ‘atachaguliwa kuongoza mwaka ujao’.

“Unabii unaweza kuchukua hata miaka 100 kabla ya kutimia na mwishowe tutashuhudia yaliyotabiriwa. Ninahimiza watu wa jamii ya Waluhya kuunga mkono Bw Odinga mwaka ujao ili awe rais wa tano wa nchi hii,” akasema.

“Ushindi wa Raila unamaanisha kwamba unabii wa Masinde kuhusu uongozi wa Waluhya utakuwa unakaribia kutimia.”

Diwani huyo ambaye anahudumu muhula wa pili, pia alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kusaidia familia ya nabii Masinde ambayo sasa inaishi maisha ya umaskini.

“Nabii alichangia pakubwa katika vita vya ukombozi wa taifa hili kutoka mikononi mwa wakoloni,” akasema. Bw Balala alisema kuwa nabii huyo alipewa jina la Elijah na jamii ya Waluhya kutokana na uwezo wake wa kutabiri mambo ambayo baadaye yalibainika kuwa kweli sawa na Nabii Eliya katika Biblia.

“Alikuwa mchezaji wa mpira kabla ya kuanzisha harakati za kupambana na wakoloni. Alikuwa na msimamo mkali na mwenye busara,” akasema.Alisema kuwa wanasiasa wengi wa jamii ya Waluhya wamekuwa wakijihusisha na nabii Masinde lakini ‘familia yake imezama kwenye umaskini’.

“Raila alifaa kuzuru kaburi la Masinde lakini kwa kuwa limechakaa, alituma vifaa vya ujenzi likarabatiwe,” akasema.

Waliotangaza azma ya kuwania urais ni Mabw Mudavadi, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Dkt Mukhisa Kituyi.

You can share this post!

Muturi aahidi vijana makuu akichaguliwa rais

Kilio familia 89 Kwale zikihofia kufurushwa