• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kingi ajitenga na lawama jukwa la mkutano wa Ruto likiharibiwa usiku

Kingi ajitenga na lawama jukwa la mkutano wa Ruto likiharibiwa usiku

Na MAUREEN ONGALA

GAVANA wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi, amejitenga na madai ya kuhusika na tukio ambapo kundi limedaiwa kukodishwa ili kuharibu jukwaa lililotarajiwa kutumiwa na Naibu Rais William Ruto, wakati wa mkutano wake katika eneo la Mbuzi Wengi, Kaunti ya Kilifi.

Jukwaa hilo pia limedaiwa kuharibiwa kufuatia mzozo wa kifamilia Alhamisi usiku.

Mkutano huo ulipangwa kufanyika saa nne za asubuhi jana Ijumaa, katika eneo hilo lililoko kando ya barabara kuu ya Kilifi kwenda Mombasa.

Kioja kilianza pale mmoja wa watu wa familia inayomiliki eneo hilo, Bw Samir Nyundo, aliposema hatakubali mkutano ufanyike hapo.

Alidai kuwa jamaa zake hawakuwa wamewaarifu kabla ya kutoa idhini ya kutumika kwa ardhi hiyo kwa shughuli za kisiasa.

Hapo ndipo anadaiwa kukodisha kundi la vijana ambao walibomoa jukwaa hilo chini ya uangalizi wake, mwendo wa saa tano za usiku.

Bw Nyundo ni mwenyekiti wa kundi la vijana wanachama wa Chama cha Pan African Alliance (PAA) katika eneo hilo.Vipaza sauti pamoja na viti pia viliharibiwa katika tukio hilo.

Hata hivyo, Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya jana Ijumaa alieleza wanahabari kwamba mkutano huo utaendelea jinsi ulivyopangwa.

“Kama wafuasi wa UDA tutaandaa mkutano hapa. Naibu Rais atahudhuria pamoja na viongozi wa vyama vya ANC na Ford Kenya. Pia kutakuwepo na zaidi ya wabunge 40,” akasema.

“Hata hivyo, kulitokea kisa cha kusikitisha ambapo wahalifu waliharibu jukwaa na kudai mkutano huo hautafanyika. Familia inayomiliki ardhi hii iliruhusu UDA kuandaa mkutano bila masharti yoyote,” Bw Baya akaongeza.

Mbunge huyo alidai kuwa kitendo hicho kilichochewa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi.

“Gavana Kingi anaogopa ushindani. Ameingiwa na uwoga kwa sababu amepoteza ushawishi. Hata hivyo, ningependa kumwambia kuwa mkutano wetu utaendelea apende asipende,” Bw Baya akasema huku akitoa wito kwa polisi kuwapa ulinzi.

Mbunge huyo alisema wakazi wa Kilifi ni watu ambao wanavumilia siasa za ushindani na “hawafai kuchochewa kuzua vurugu zisizo na maana.”

“Watu wa Kilifi wamekomaa kisiasa na wanataka kuruhusiwa kushindana kwa usawa,” Bw Baya akasema huku akilaumu machifu wa eneo hilo kwa kuunga mkono uhalifu.

Hata hivyo, Gavana Kingi alijitenga na madai kuhusiana na tukio hilo akisema hana sababu maalum ya kuvuruga mkutano wa Naibu Rais.

“Mbona nihujumu mkutano wa Naibu Rais wakati huu ilhali awali amekuwa akifanya mikutano mingi katika kaunti hii ya Kilifi bila tatizo lolote?” Gavana Kingi, ambaye yuko Nairobi kwa shughuli za kikazi, akasema.

  • Tags

You can share this post!

Western Sahara: Kenya yataka AU ijadili mzozo

DOUGLAS MUTUA: Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarishwe...

T L