• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Western Sahara: Kenya yataka AU ijadili mzozo

Western Sahara: Kenya yataka AU ijadili mzozo

Na AGGREY MUTAMBO

NAIROBI, KENYA

KENYA imeshinikiza viongozi wa mataifa ya Afrika kujadili tena mzozo kuhusu umiliki wa eneo la Western Sahara ambalo Morocco inashikilia kuwa ni sehemu yake.

Kenya ambayo mwezi huu ni mwenyekiti wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Mataifa (PSC), inataka viongozi wa mataifa wanachama ya Umoja wa Afrika (AU) kujadili tena mzozo kuhusu umiliki wa eneo la Western Sahara.

Kulingana na Kenya, mvutano kuhusu umiliki wa eneo hilo umekuwa ukizua mapigano ya mara kwa mara.Kenya inataka suala hilo lijadiliwe katika mkutano wa viongozi wa Afrika utakaofanyika kwa njia ya mtandao Februari 16, 2022.

Morocco inashikilia kuwa eneo la Western Sahara ambalo awali lilijulikana kama Sahrawi Arab Democratic Republic ni sehemu ya nchi yake.

Lakini Kenya inataka wakazi wa Western Sahara wajiamulie, kupitia kura ya maamuzi, ikiwa watakuwa sehemu ya Morocco au itakuwa nchi huru.

Kwenye mkutano wa PSC uliofanyika Machi 2021, na kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, ulitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano Western Sahara na kumtaka balozi wa AU katika eneo hilo, Joachim Chissano, kushawishi pande husika kukubali kupatanishwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Mkutano huo pia ulihimiza Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, kuteua balozi wa kusaidia kuleta amani katika eneo la Western Sahara.

Guterres alimteua raia wa Italia, Staffan de Mistura, kuwa balozi wa UN katika eneo la Western Sahara.

Kenya inashikilia kuwa mzozo kuhusu eneo hilo unatatiza maendeleo na amani katika mataifa ya ukanda wa Maghreb.Mwaka jana, waziri wa masuala ya kigeni wa Morocco Nasser Bourita aliandikia barua Kenya akisema suala la mzozo kuhusu umiliki wa eneo la Western Sahara linafaa kuepukwa.

“Kujadiliwa kwa suala hilo kutazua mgawanyiko miongoni mwa mataifa wanachama wa PSC. Kuna masuala mengine nyeti ya kujadiliwa kama vile janga la virusi vya corona,” akasema Bourita kupitia barua hiyo aliyoandika mnamo Machi 1.

Morocco inataka mzozo huo utatuliwe UN pamoja na wenyekiti wa zamani wa AU; wanaojumuisha marais Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Felix Tshisekedi (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na Macky Sall (Senegal).

Eneo la Western Sahara lilikuwa likitawaliwa na Uhispania lakini baadaye lilitwaliwa na Morocco.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lilipendekeza kufanyika kwa kura ya maamuzi ili wakazi wajiamulie ikiwa wanataka kuwa chini ya Morocco au kuwa nchi huru.

AU pia iliunga mkono pendekezo hilo la UN lakini kufikia sasa kura ya maamuzi haijaandaliwa.

Mnamo 2020, aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump alitangaza kuwa eneo la Western Sahara ni sehemu ya Morocco.

Tangazo hilo la Trump, hata hivyo, lilipingwa vikali na Umoja wa Afrika ambao ulisema mzozo huo ulistahili kutatuliwa kupitia kura ya maamuzi kama ilivyopendekezwa na UNSC.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuhutubia kongamano la 35 la viongozi wa Umoja wa Afrika, kesho, ambapo anatarajiwa kuzungumzia masuala ya amani, ugaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

You can share this post!

Kura: Korti yaongeza muda wa kujiuzulu

Kingi ajitenga na lawama jukwa la mkutano wa Ruto...

T L