• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
DOUGLAS MUTUA: Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarishwe kuzima uhalifu

DOUGLAS MUTUA: Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarishwe kuzima uhalifu

NA DOUGLAS MUTUA

KADIRI Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inavyozidi kupanuka ndivyo ninavyotambua manufaa yake. Mathalan, wahalifu wa kimataifa wanajiuliza watakuwa wageni wa nani!

Kisa na maana? Mataifa yote wanachama ama yatakuwa na mikataba ya kubadilishana watuhumiwa wa uhalifu, au wahalifu watafungwa gerezani watakakotenda maovu yao.

Unaiposoma makala hii, mfanyabiashara wa kimataifa, Bw Nathan Loyd Ndung’u, ameketi korokoroni akisubiri mahakama iamue iwapo atakabidhiwa serikali ya Rwanda.

Alikamatwa hivi majuzi baada ya kuikwepa serikali ya Rwanda kwa mwongo mzima; mahakama ya taifa hilo ilimpata na hatia ya ulaghai mnamo 2012.

Mashtaka dhidi yake ni kwamba aliuza ardhi isiyokuwa yake nchini humo kisha akachana mbuga.

Alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani.

Na kwa kuwa Bw Ndung’u hakuwa mahakamani wakati wa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi yake, Rwanda iliwasiliana na polisi wa kimataifa, Interpol, akatiwa mbaroni juzi.

Kisa cha Bw Ndung’u kimetokea siku chache tu baada ya kingine ambapo gaidi Mkenya, Salim Rashid Muhamed, alikamatwa ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Sasa Kenya na DRC zinashauriana kuhusu anakopaswa kushtakiwa kwa kuwa ni mtoro nchini Kenya, hali huko DRC anatuhumiwa kuchinja mtu hadharani eti kwa kuwasaliti magaidi!

Nasisitiza wahalifu watakosa kwa kutorokea kwa kuwa ushirikiano wa mataifa wanachama wa EAC unaonekana kutowapendelea watundu.

Hakuna taifa linalowatetea raia wake kwa vyovyote vile wakivunja sheria kotekote.

Je, unamkumbuka marehemu Rais wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli, akishangilia kufungwa jela nchini Kenya kwa Mtanzania Rashid Charles Mberesero?

Mberesero ni mmoja wa magaidi waliovamia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua wanafunzi 148 mnamo mwaka 2015.

Gaidi huyo alipofungwa maisha, Rais Magufuli alishangilia kwa kusema Tanzania haihitaji watu kama hao.

Hatimaye gaidi wa watu alijitia kitanzi! Mwoga wa mwisho!

Vilevile, mwanasiasa na mfanyabiashara Mkenya, Don Bosco Gichana, alipotuhumiwa kulaghai watu na kutakatisha pesa, Tanzania ilimfunga jela miaka mitano na ushei!

Je, unawakumbuka Wakenya wanne waliofungwa maisha nchini Uganda kwa kufanya mashambulio ya kigaidi huko wakati wa fainali za Kombe la Dunia mnamo mwaka 2010?

Usijilaumu.

Hata Serikali ya Kenya imewasahau. Mahakama iliwahukumu kwa kuwaua watu wasiokuwa na hatia 76 na kuwajeruhi wengine.

Kuna kisa ambapo aliyekuwa Rais wa DRC, Joseph Kabila, alitinga nchini Kenya kwa dharura kumlalamikia mwenzake, Mwai Kibaki, kuhusu dhahabu iliyoibwa DRC.

Ushirikiano wa EAC ungekuwa umeiva, labda Mkenya aliyetuhumiwa kuiba dhahabu hiyo ya mabilioni ya pesa angerejeshwa DRC akakabiliwe na sheria.

Ikiwa ushirikiano huo utasaidia kupunguza uhalifu, hasa wizi wa magari na madini, basi na uimarishwe kabisa, tena kwa kasi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kingi ajitenga na lawama jukwa la mkutano wa Ruto...

Uhuru ataja mbinu za kuvumisha Raila

T L