• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Kocha aliyechagua kufunza uwanjani badala ya darasani

Kocha aliyechagua kufunza uwanjani badala ya darasani

Ingawa alifuzu kuwa mwalimu wa darasani kutoka Chuo Kikuu cha ZETECH, kocha Dickson Amugasha aliamua kuelekeza mafunzo viwanjani kama mnoaji.

Anasema baada ya kuhitimu, alifanya kazi ya ualimu kwa muda mfupi kisha moyo wake ukamdekadeka kurudishia mkono jamii kupitia mwanya wa kukuza talanta za vijana viwanjani. Shule ya mwisho ilikuwa Kangemi Youth Centre.

Anadokeza kwamba, aliamini kujenga msingi bora wa jamii kwahitaji vijana wawe katika mkondo wa nidhamu, maadili mema na kutumia muda wao vyema kwa kuzingatia masuala ya kuinua jamii kupitia michezo.Kupitia ari yake ya kukuza vipaji, mkufunzi huyo aliamua kujenga timu ya Young City ambayo maskani yake yako uwanjani Kihumbuini, Kangemi mwaka wa 2016.

Hata hivyo, kabla kujenga msingi wa timu hii, alikuwa ameifunza timu ya Kibagare City kwa kipindi kifupi.Anasema timu hii, aliianza kama akademia ya soka ambayo ilijumuisha wachezaji 40 ambao walikuwa wanafunzi wa shule za msingi mtaani Kangemi na mingine jirani.

Chipukizi hao wamelelewa vipawa na vimekuwa vya kufaidi kwao. Vimefungulia baadhi yao milango ya masomo kupitia udhamini wala timu zingine kunufaika na wanatalanta hao.Kocha Amugasha aliye mfadhili wake, ameihimili timu hii kwa hali na mali licha ya kukumbana na changamoto si haba.

Anaeleza licha ya kuwa na hamu na ghamu kuona wahisani wakijitokeza kumpiga jeki, visiki vya kuvikuza vipaji bado vingalipo! Inambidi awasajili wachezaji na kuwasaidia kupata upenyu masomoni kwa sababu kama mwalimu anaamini masomo ni kifunguo cha maisha!

Isitoshe, kujisajili kwenye ligi, usafiri na ada za marefa ni miongoni tu mwa mahitaji mengine ya timu hadi sasa amabayo ni kuzungumti kuyagharimia. Wachezaji ambao alianza nao, wengi wangali na timu. Wengine wamemaliza shule akiwemo Brian Machisu ambaye alisomea Shule ya Dagoretti High na kuna Straika Daniel Mudegu ambaye yuko katika kidato cha tatu shule iyo hiyo akijituma masomoni na kusakata kandanda.

Mbali na wengine wengi walio shule mbalimbali.Baada ya kuvichochea vipaji hivi hadi vikawa vimekomaa kushiriki ligi, (ya wasiozidi miaka 17) alianza kuvishirikisha katika Ligi ya Shirikisho la Soka Kenya, tawi la Nairobi West mwaka wa 2017 na 2018.

Vilionesha weledi wa kusakata kabumbu kwa kuwa katika nafasi ya sita na tatu mtawalia kisha kupandishwa ngazi ya Ligi ya Kaunti, msimu ambao ulisisitishwa kutokana na msambao wa corona japo ilishikilia nafasi ya nne ligini.

Kwa vile nia yake kustawisha timu ilikuwa kuifaulisha ipande ngazi na wachezaji kupokea jukwaa lifaalo la kujikuza, kuna wanasoka ambao wamepitia mikononi mwake na wanachezea timu kama Gor Mahia Youth ambapo kiungo Brian Oluoch na difenda Jamin Isindu wamesajiliwa.

‘Nafurahia ninapoona vipaji ambavyo nimechonga vikionyesha ustadi wa soka katika majukwaa mbalimbali na bado vingine vingali katika ufinyanzi,” anasema.kocha huyo ambaye anakuza timu kupitia mashauri nasaha na uhusiano mwema wakati anawanoa wanadimba hao.

Isitoshe, anajikaza kisabuni katika safari ya kujenga msingi wa wanavipaji hao hadi wahisani na wafadhili watapojitokeza kuiunga mkono. Angependa kuwasihi wahisani wa soka kujitokeza kuisadia timu kwani anaamini umoja ni nguvu.

Na kusisitiza kwamba, vipawa vya soka ni riziki na vipo mashinani ila, kuvikuza ni gharama!

  • Tags

You can share this post!

Polio: Wazazi wahimizwa kuwapeleka watoto wao kwa chanjo

Wasafiri 7 kutoka Tz waponea baada ya boti lao kuzama