• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Kocha Vihiga Queens asema hakuna kulaza damu Ligi kuu

Kocha Vihiga Queens asema hakuna kulaza damu Ligi kuu

Na JOHN KIMWERE

KAMPENI za kuwania taji la Ligi Kuu ya Soka la Wanawake zinaendelea kuchacha huku Vihiga Queens ikizidi kukaa kileleni baada ya kupiga mechi saba.

Vihiga Queens ya kocha, Boniface Nyamunyamu ilizaba Zetech Sparks 5-0, Gaspo Women ililima Wadadia FC 2-1 nayo Ulinzi Starlets ilipanda hadi nafasi ya tatu ilipozoa 5-1 mbele ya Trans Nzoia Falcons. Kangemi Starlets iliendelea kuambulia patupu ilipokubali kulala kwa 4-0 mbele ya Thika Queens. Nayo Kayole Starlets ilinyukwa 4-0 na Bunyore Starlets.

”Nataka vipusa wangu waelewe kuwa hakuna kulaza damu bali tuzidi kupiga shughuli kibabe dhidi ya wapinzani wetu ili kujiweka pazuri kubeba taji,” kocha wa Vihiga anasema. Wafungaji wa Vihiga Queens:Christine Nafula na Tereza Engesha kila mmoja alitikisa wavu mara mbili naye Lorna Nyarinda alifunga goli moja.

Nao Mercy Airo na Corazone Aquino kila mmoja alifungia Gaspo Women bao moja na kusaidia kutia alama tatu kapuni. ”Bila shaka tuna kibarua kigumu ilhali tumepania kubeba taji la muhula huu,” kocha wa Gaspo, Domitila Wangui alisema na kuongeza kuwa wanataka taji la muhula huu.

Wachezaji wa Ulinzi wakisherekea baada ya kufunga wenzao kwenye mechi ya kipute cha KWPL…Picha/JOHN KIMWERE

Marvecyl Simiyu alijifunga na kusaidia Ulinzi kupata bao la kwanza dakika ya 21. Hata hivyo vipusa wa Ulinzi Starlets walikaza buti na kufanya kweli kupitia Lanoline Aoko, Siliya Rasoha, Gentrix Kuyudi na Sheril Andiba waliofunga bao moja kila mmoja.

Trans Nzoia chini ya nahodha, Martha Amunyolete ilipata bao la pekee kupitia juhudi zake Joyce Makungu. Vihiga inaongoza kwa alama 19, tatu mbele ya Gaspo Women. Ulinzi ya tatu kwa alama 14 nazo Trans Nzoia Falcons na Thika zinashikilia nafasi ya nne na tano mtawalia.

Kocha wa Trans Nzoia Falcons, Justine Okiring akiongea na wachezaji walipocheza na Ulinzi Starlets kwenye mechi ya Ligi Kuu (KWPL) ugani Ruaraka, Nairobi. Ulinzi ilishinda mabao 5-1…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Watu saba wafariki dunia baada ya matatu kukanyaga kilipuzi...

Wabunge kurejea bungeni kesho kujaribu kuokoa jahazi la...

T L