• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:52 PM
Wabunge kurejea bungeni kesho kujaribu kuokoa jahazi la uundwaji wa HBC

Wabunge kurejea bungeni kesho kujaribu kuokoa jahazi la uundwaji wa HBC

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wanarejea bungeni Jumanne, Februari 1, 2022 wiki moja baada ya wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza kuzima uteuzi wa wanachama wa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge (HBC).

Kiongozi wa wengi Amos Kimunya Alhamisi wiki jana alishawishi Spika Justin Muturi kuitisha kikao cha bunge ili kubatilisha uamuzi wa kukataliwa kwa orodha ya wabunge saba walioteuliwa kuhudumu katika kamati hiyo ya HBC.

Jumanne wiki jana Spika Muturi alilazimika kusitisha vikao vya Jumatano na Alhamisi baada ya wabunge hao wandani wa Naibu Rais William Ruto kuangusha hoja ya kuundwa kwa kamati ya HBC.

Kulingana na sheria ya bunge nambari 49, bunge la kitaifa huunda upya kamati ya HBC na kamati nyingine za awamu, kila mwaka bunge linaporejelea vikao.

HBC huongozwa na Spika Muturi na ndio yenye mamlaka ya kuratibu shughuli za kujadiliwa bungeni kila wiki.

Kamati hiyo ndio hutengeneza taarifa zenye ajenda za kujadiliwa bungeni maarufu kwa kimombo kama Order Paper.

Ikiwa wabunge watafeli kubatilisha hoja ya kuundwa upya kwa HBC, bunge haliwezi kufanya vikao kwa muda wa miezi sita ijayo, hali ambayo itaathiri shughuli muhimu za kitaifa kama utayarishaji wa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Kuanzia wiki hii wabunge wanatarajiwa kuanza kutayarisha Bajeti ya Ziada na Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023 unaoanza Julai 1, 2022 kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kamati ya HBC pia huandaa ratiba ya Bunge la Kitaifa na huamua miswada na hoja za kupewa kipaumbele.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Vihiga Queens asema hakuna kulaza damu Ligi kuu

Wanakarate wa Zetech kupandishwa gredi

T L