• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
KRU kuleta mastaa wa Kenya Simbas mechi za kuingia Kombe la Dunia 2023 zikinukia

KRU kuleta mastaa wa Kenya Simbas mechi za kuingia Kombe la Dunia 2023 zikinukia

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) linafanya mipango kuleta wachezaji wanne wa kimataifa kupiga jeki timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande inayojiandaa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2023.

Kocha wa timu hiyo maarufu kama Simbas, Paul Odera aliambia Taifa Leo kuwa ameomba KRU wachezaji Malcom Onsando (Romania), Andrew Siminyu (Afrika Kusini) na ndugu Jeff Mutuku na Mark Mutuku (Amerika).

“Kumekuwa na changamoto ya kupata tiketi za wachezaji hao kutoka wanakocheza. Nimeomba KRU ijaribu kuwaleta kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia zitakazoanza mwezi ujao wa Julai,” alisema Odera.

Hata hivyo, mwalimu huyo wa shule ya Peponi House Preparatory jijini Nairobi alisema kuwa matumaini yake ya kupata wachezaji hao ni madogo. Hii ni baada ya Simbas kushindwa kusafiri nchini Afrika Kusini kwa kambi ya mazoezi na mechi za kujipima nguvu kutokana na ukosefu wa fedha. Simbas iliratibiwa kumenyana na wenyeji wa kambi hiyo Stellenbosch mnamo Juni 18, siku tatu baada ya kuchuana na Helderberg.

Odera alifichua kuwa maskauti kutoka Uingereza na Afrika Kusini walipanga kuhudhuria kambi ya Simbas kwa lengo la kupendekeza wachezaji kadhaa wazuri kuajiriwa katika klabu za kigeni.

“Ni bahati mbaya kwetu na pia wachezaji waliotumai wataonekana na kuridhisha maskauti,” alisema.

Simbas itaalika Uganda kwa mechi ya Kombe la Elgon hapo Juni 26. Inatetea taji la Elgon Cup baada ya kushinda makala yaliyopita mwaka 2019. Ilishinda kwa jumla ya alama 29-21 baada ya kuchapwa na Cranes 16-13 Juni 22 ugani Mamboleo mjini Kisumu na kulipiza kisasi dhidi ya wenyeji wao 16-5 mjini Kampala mnamo Julai 13.

Baada ya Elgon Cup, Simbas itaalika Senegal mnamo Julai 3 na Zambia mnamo Julai 11. Mshindi wa raundi hiyo ya kwanza ya mataifa hayo matatu ataweka hai matumaini ya kuingia Kombe la Dunia 2023 kwa sababu atashiriki mashindano ya mwisho ya kufuzu mwaka 2022.

  • Tags

You can share this post!

SUPALIGI YA TAIFA: Coast Stima yapoteza mechi ya tatu...

Bandari FC iko tayari kuishinda Equity FC mechi ya nusu...