• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
MKU na Unesco kushirikiana kufanikisha mradi wa afya wa o3 Plus

MKU na Unesco kushirikiana kufanikisha mradi wa afya wa o3 Plus

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya kinashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kufanikisha mradi wa afya wa Our Rights, Our Lives, Our Future (O3 Plus) yaani Haki Zetu, Uhai Wetu na Mustakabali Wetu.

Ushirikiano huo pia umejumuisha Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo pia kutakuwa na ushirikiano na vyuo vingine vya humu nchini.

Mradi huo unanuia kuona ya kwamba wanafunzi wanajali hali yao ya kiafya na kimaisha kwa kujiepusha na maswala maovu yanayoweza kudhuru afya yao.

O3 Plus ni mradi unaolenga kuhakikisha kwamba vijana wanapata hamasisho kujiepusha na mienendo hatari hivyo kupunguza maambukizi ya Ukimwi, wawe na afya nzuri, kusawazisha uwakilishi wa kijinsia pamoja na kuepuka dhuluma za kijinsia ikiwemo vurugu dhidi ya jinsia fulani.

Pro-Chansela wa MKU Dkt Vincent Gaitho, alisema wazazi, na wahadhiri popote pale walipo wana nafasi njema ya kuwahamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu ili wasije wakapotoka.

“Nyinyi vijana mnahitaji mawaidha ya kila mara ili msipotoke na kufikia utu uzima mkiwa wakomavu,” alifafanua Dkt Gaitho.

Aliwashauri wanafunzi wa MKU wawe makini wasije wakapotoshwa na dhoruba kali kutoka nje.

Alisema kuna maradhi hatari ya zinaa, maswala ya akina dada kupachikwa mimba za mapema, na dhuluma za kimapenzi.

Vijana wengi wametumbukia katika mitego hiyo bila kuelewa madhara yake. Kwa hivyo ni vyema kuwa macho ili msipotoshwe kwa majaribio ya aina yoyote,” alisema Dkt Gaitho.

Aliwatahadharisha kuwa makini ili wasiingilie dawa za kulevya na kuwataka kujiepusha na fujo za kimapenzi.

Alisema wasichana wengi huingilia maswala ya ngono bila kuelewa madhara yake. Pia wengine wanaingilia ulevi na mapenzi kiholela.

Mwanzilishi wa MKU Dkt Jane Nyutu, aliwahimiza wanafunzi kuzingatia mradi huo muhimu uliozinduliwa kwa sababu uakuwa wa manufaa kwao.

Alisema chuo hicho kitafanya juhudi kushirikiana pamoja na vyuo vingine ili kufanikisha malengo ya mradi huo.

Aliwataja Dkt Mary Mugwe na Prof Kennedy Mutundu kama watu wenye maono ambao wamekuwa mstari wa mbele kufanikisha malengo hayo.

Naye Naibu Chansela wa chuo hicho Prof Deogratius Jaganyi alisema wanafunzi wanapitia changamoto tele lakini akawapongeza kwa kufuatilia kwa karibu mradi huo.

Aliwaonya wanafunzi wasiingilie mapenzi yasiyo na ushirikiano mzuri kwani yanaleta vurugu.

“Iwapo huelewani na rafiki yako achana naye na uendelee mbele na maisha yako. Usiwe mtumwa wa mapenzi,” alishauri msomi huyo.

Alisema mbali na Kenya, mradi huo pia utaendeshwa Tanzania, Zambia na Zimbabwe, ili wanachuo katika nchi hizo waafikie malengo yao ya siku zijazo.

You can share this post!

ODM Magharibi wataka tiketi ya Raila-Oparanya

Majaji: Uhuru ashinda raundi ya kwanza

T L