• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
ODM Magharibi wataka tiketi ya Raila-Oparanya

ODM Magharibi wataka tiketi ya Raila-Oparanya

Na SHABAN MAKOKHA

KINARA wa ODM Raila Odinga anakabiliwa na kibarua kigumu cha kumteua mgombeaji mwenza wake huku wandani wake kutoka eneo la Magharibi wakimtaka ampe Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya nafasi hiyo kuelekea kura ya 2022.

Wanasiasa kutoka eneo la Pwani na Mlima Kenya nao pia wamekuwa wakimshinikiza waziri huyo mkuu wa zamani awakabidhi nafasi hiyo, wakati ambapo anaonekana kuungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Hapo Jumapili, mbunge wa Shinyalu Justus Kizito ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM katika Kaunti hiyo, alisema kuwa Bw Oparanya anatosha kuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga kwa kuwa ana uwezo wa kumvutia kura zote za eneo hilo.

Akiwa ameandamana na Mbunge Mwakilishi wa Kike Elsie Muhanda na Seneta Maalum Naomi Shinyonga, Bw Kizito alimkumbusha Bw Odinga kuwa wakati wa mkutano wa wajumbe wa ODM wiki moja iliyopita, iliamuliwa kuwa nafasi hiyo iende kwa Bw Oparanya.

Wajumbe hao walitoka katika kaunti tano za eneo hilo za Bungoma, Busia, Vihiga, Trans Nzoia na Kakamega.

Walisema kuwa Bw Oparanya amekuwa mwaminifu kwa Bw Odinga tangu 2002 na hata ametupilia mbali azma yake ya kuwania kiti cha urais ili kuunga mkono kigogo huyo wa siasa za upinzani.

“Kando na kuwa mwanasiasa wa ngazi ya juu katika ODM, Oparanya amemuunga mkono Raila miaka hii yote na anatosha kushikilia wadhifa wa Naibu Rais,” akasema Bi Shiyonga.

Bw Kizito naye alifichua kuwa gavana huyo anayehudumu muhula wake wa pili, alikuwa ameweka mikakati ya kuvumisha ODM Magharibi ili irejelee umaarufu wake wa zamani ndipo ishinde viti vingi katika gatuzi hilo.

Mnamo Oktoba 27, Bw Oparanya aliwapokea wazee kutoka Baraza la Wazee wa jamii ya Bukusu nyumbani kwake kijiji cha Mabole ambapo waliahidi kuwa wataunga mkono azma ya Bw Odinga.

Kauli ya wanasiasa kutoka Magharibi sasa inamweka Bw Odinga katika njia panda huku akijiandaa kupambana na Naibu Rais Dkt William Ruto kuwa rais wa tano wa nchi.

Ikikisiwa kuwa uwaniaji wa Bw Odinga unaungwa mkono na Rais Kenyatta, madai yamekuwa yakienea kuwa Naibu wake atatoka Mlika Kenya.

Nao viongozi wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wamekuwa wakishinikizwa wamuunge mkono Bw Odinga na kuibua madai kuwa atateua mmoja wao kuwa mgombeaji mwenza wake.

Mchanganuzi wa kisiasa Martin Andati anasema kuwa Bw Odinga ana maamuzi magumu ya kumteua mwaniaji mwenza wake japo anasema kuwa iwapo OKA wataendelea na mipango yao ya kuwania urais, basi Bw Oparanya au Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua wanatosha kuchukua nafasi hiyo.

“Kumchagua mwaniaji mwenza ni kibarua kigumu kwa Raila hasa wakati huu ambapo ameanza kupata uungwaji mkono Mlima Kenya. Pia lazima amakinike kuhakikisha Magharibi haikosi nafasi kutokana na idadi kubwa ya wapigakura wake wengi,” akasema Bw Andati.

Hata hivyo, Bw Oparanya wiki jana alisema kuwa kiongozi wa chama chake anafaa kumteua mwaniaji mwenza kutoka Mlima Kenya kwa kuwa haitaonekana vyema kwa Rais na Naibu wake kutoka Nyanza na Magharibi mtawalia.

You can share this post!

Vyama vidogo vinachochea chuki na ukabila, Ruto adai

MKU na Unesco kushirikiana kufanikisha mradi wa afya wa o3...

T L