• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Kukubo angali na ndoto ya kuwa rais wa Kenya

Kukubo angali na ndoto ya kuwa rais wa Kenya

Na WINNIE ONANDO

ALIYEKUWA mwanajeshi katika Kikosi cha ulinzi cha KDF, Nixon Kukubo aliyewania kiti cha urais mara mbili na kushindwa ametangaza azimio lake la kuwania kiti hicho mara nyingine.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Kukubo aliyepata kura 5,927 katika uchaguzi wa 2007 alisema kuwa yupo tayari kukabiliana na kinara wa ODM, Raila Odinga na Naibu Rais, William Ruto.

“Bado ninaamini mimi ndiye mwanasiasa sahihi kuchaguliwa kuwa rais wa Kenya. Wakenya wanahitaji kukombolewa kutoka kwa viongozi wa sasa ambao ni wafisadi,” akasema Bw Kukubo.

Mzee huyo wa miaka 64 ambaye kwa sasa ni mwanamuziki anawalaumu viongozi wa sasa wanaozunguka wakitoa ‘ahadi hewa’ kwa Wakenya kuwa wamechangia pakubwa katika kuzorota kwa hali ya uchumi nchini.

“Sasa hivi wanazunguka wakitoa ahadi ambazo hawatatimiza. Ni viongozi wale wale ambao wameshindwa kuwatumikia Wakenya.”

Alisema viongozi wa sasa wanapaswa kujiuzulu na kuwaachia watu wapya ambao wametangamana na wananchi na kuelewa hali jinsi ilivyo.

“Mtu kama Jimmi Wanjigi hajawahi kujihusisha na siasa. Naomba tuungane naye ili tuunde serikali itakayomfaidi mwananchi wa kawaida. Wakenya wanapaswa kuwachagua wawaniaji wapya ili kuwaondoa walio uongozini sasa.”

Alisema akichaguliwa kama rais katika uchaguzi mkuu mwaka ujao, atatoa uongozi bora na usio na ufisadi.

Alisema amalenga kuzindua rasmi azma yake ya kuwania urais Februari 2022 katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

“Wakati wa uzinduzi, zaidi ya watu 33,000 watahudhuria. Katika kila kaunti, tutakuwa na wawakilishi 20.”

Kupitia chama chake cha Tumaini Liberation, Bw Kukubo ana imani kuwa atamaliza umaskini na njaa nchini.

Alijihisisha na masuala ya kisiasa mwaka wa 2001.

You can share this post!

Ruto awasuta wanaotaka ajiuzulu

Bunge lasitisha shughuli Uganda kufuatia milipuko ya mabomu

T L