• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Maandamano ya Azimio: Mathare, ni mguu niponye waandamanaji wakikabiliana na polisi

Maandamano ya Azimio: Mathare, ni mguu niponye waandamanaji wakikabiliana na polisi

NA NYABOGA KIAGE

MTAA wa mabanda wa Mathare, Nairobi taswira Jumatano, Julai 12, 2023 ni ya mguu niponye kufuatia makabiliano makali yanayoshuhudiwa kati ya polisi na waandamanaji wa Azimio la Umoja.

Kitongoji cha Nabatini, mtaani humo maafisa wa polisi wamelazimika kutumia gesi ya vitoa machozi kutawanya makundi ya waandamanaji wanaowasha magurudumu barabarani, ikiwemo Juja.

Mwandamanaji Mathare aliyejeruhiwa. Picha|NYABOBA KIAGE

Maandamano ya kitaifa ya Azimio yamelinagana na ya wahudumu wa matatu na teksi, wanaopinga ada ya Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama wa Kitaifa (NTSA) madereva kulipia upya mafunzo kupima uhalisia wao kuwa barabarani.

Huduma za usafiri na uchukuzi Mathari zimeathirika, ikizingatiwa kuwa eneo hilo ni mojawapo wa ngome za kinara wa Azimio Bw Raila Odinga.

Kufuatia mfarakano kati ya askari na wafuasi wa Azimio, mwandamanaji mmoja amejeruhiwa na kupelekwa hospitalini kupata matibabu ya dharura.

Maandamanaji hayo yalipigwa marufuku na Inspekta Jenerali wa Polisi IG Japheth Koome.

Mojawapo ya gesi ya kutoa machozi iliyorushiwa waandamanaji na polisi mtaa wa Mathare, Nairobi. Picha|NYABOGA KIAGE

Odinga ameyatetea akihoji yanalenga kushinikiza serikali kushusha gharama ya juu ya maisha, japo Bw Koome alisema kuwa viongozi wa upinzani hawakuwa wameomba ruhusa kuyatekeleza.

Alisema kuwa kundi la upinzani halitakubaliwa kufanya maandamano hayo mahali popote nchini.

“Kwa sababu ya usalama wa umma, polisi wameamua kuwajulisha wananchi kuwa hakuna maandamano yatakayoshuhudiwa Jumatano (Julai 12, 2023). Polisi watafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa kuna usalama,” Bw Koome alisema.

Barabara ya Thika Superhighway, magari yalikuwa machache kufuatia hofu ya zogo la maandamano.

Mojawapo ya barabara Mathare, Nairobi huduma za usafiri na uchukuzi zimepungua kufuatia maandamano ya Azimio. Picha|NYABOGA KIAGE

 

  • Tags

You can share this post!

Itumbi akata rufaa kupinga kuharamishwa kwa nyadhifa 50 za...

Raila: Maandamano kote nchini ni ujumbe tosha kwa Ruto

T L