• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Raila: Maandamano kote nchini ni ujumbe tosha kwa Ruto

Raila: Maandamano kote nchini ni ujumbe tosha kwa Ruto

NA JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga amesema maandamano yanayoendelea kote nchini yanafikisha ujumbe kwa utawala wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais Dkt William Ruto.

Akihutubu katika ukumbi wa Jaramogi Oginga Odinga Foundation (JOOF) jijini Nairobi mnamo Jumatano, Bw Odinga amesema Wakenya wengi wamelemewa na gharama ya juu ya maisha.

Na wakati huo huo, Bw Odinga amedai kwamba jana Jumanne usiku Azimio walipata dokezi za kuwepo kwa njama ya Kenya Kwanza kukomboa wakora kuwapiga risasi viongozi na waandamanaji ambao wangejitokeza katika uwanja wa Kamukunji huku wakora hao wakilindwa na maafisa wa polisi. Ni kwa sababu hiyo ndipo akasitisha mkutano uliofaa kuandaliwa uwanjani Kamukunji leo Jumatano.

“Ukweli ni kwamba maandamano kote nchini yanaonyesha wazi kwamba Wakenya wamelemewa na ugumu wa maisha,” amesema Bw Odinga.

Amewalaumu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kuwaumiza waandamanaji ambao “kosa lao pekee ni kuonyesha wazi kutoridhishwa kwao na serikali ya Kenya Kwanza.”

Aidha, Bw Odinga amesema hakuna kulegeza kamba hadi “Ruto aonyeshe yuko tayari kuwasikia Wakenya kujua matakwa yao na kuwaheshimu.”

“Ni sharti mjitokeze kutetea haki yenu kwa sababu Ruto akiachwa kusukuma mbele Sheria ya Fedha ya 2023 itakuwa ni kawauda kwa Wakenya kuteseka,” amesema Bw Odinga.

Anataka kiongozi wa nchi ajitokeze kuhakikisha vifungu tata vinang’olewa kwenye Sheria ya Fedha ya 2023 ili gharama ya maisha irudi chini.

Kuhusu suala la uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kiongozi huyo wa upinzani amesema ni sharti Dkt Ruto akubali majadiliano ya wazi ya wawakilishi kutoka Azimio na Kenya Kwanza kupata suluhu kwa maswala tata.

“Kwa umoja na ushirikiano tunaoonyesha, Ruto atakubali kuwapa Wakenya dili nzuri,” ameongeza.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano ya Azimio: Mathare, ni mguu niponye waandamanaji...

Maandamano: Raila adai serikali imetuma wahuni kuvuruga...

T L