• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Mabilioni yamwagika kukabili mabadiliko ya tabianchi Afrika

Mabilioni yamwagika kukabili mabadiliko ya tabianchi Afrika

NA MARY WANGARI

MATAIFA barani Afrika yakiongozwa na Kenya huenda yakanufaika pakubwa kutokana na uwekezaji wa mabilioni ya pesa kutoka Uingereza unaolenga kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi barani humu.

Huku kongamano la kwanza kabisa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi kuwahi kufanyika Afrika likianza rasmi jijini Nairobi hapo jana, Uingereza imetangaza uwekezaji wa Sh9bilioni.

Fedha hizo zinadhamiriwa kuanzisha miradi mipya itakayopiga jeki juhudi za kuhifadhi mazingira na kuwezesha jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kupitia Wizara inayosimamia Maendeleo Afrika, Uingereza vilevile imeahidi kujitolea kwake kufanikisha mkataba wa kimataifa wenye thamani ya Sh2 trilioni wa kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kipindi cha miaka mitano.

Fedha hizi zinajumuisha Sh6.2 bilioni zitakazotumika kuanzisha miradi mipya katika mataifa 15 ya Afrika kwa lengo la kusaidia wanawake, jamii zilizo hatarini, na wakulima zaidi ya 400,000, alisema Waziri wa Uingereza anayesimamia Maendeleo Afrika, Andrew Mitchell katika ufunguzi wa kongamano hilo.

Wanajamii wanaoishi mashinani vilevile huenda wakapata afueni kupitia mifumo ya kutoa ilani mapema kama vile jumbe za simu, mitandao ya radio na ya kijamii ili kuwawezesha kuwasiliana na kuchukua hatua mapema kabla ya majanga kutokea.

Waziri alisema miradi hiyo mpya itaboresha raslimali za maji zitakazofaidi wanajamii zaidi ya 1.5 milioni.

 

Uwekezaji Afrika

Sekta ya biashara barani inatazamiwa kunufaika vilevile kutokana na miradi mipya saba yenye thamani ya Sh2.7 bilioni iliyozinduliwa na Uingereza kupitia shirika la kufadhili uwekezaji Afrika (FSD).

Wawekezaji sasa wataweza kupata mtaji kutoka kwa mashirika ya kibinafsi na kuunda bidhaa za kibunifu zinazojumuisha teknolojia kama vile kugeuza jangwa kuwa ardhi ya kilimo.

Kwa jumla, maelfu ya Waafrika wanatazamiwa kunufaika kutokana na nafasi 3,400 za ajira na kusambaziwa umeme kupitia miradi hii mipya inayotazamiwa kuboresha huduma za kimsingi ikiwemo nishati.

“Ushirikiano wetu na nchi za Afrika kuhusu uwekezaji wa nishati salama kwa mazingira na mifumo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unakuza mifumo ya uchumi na kuboresha maisha. Lakini hatua zaidi ni sharti zichukuliwe kwa sababu wale wasiochangia pakubwa katika mabadiliko ya tabanchi wanazidi kuathirika zaidi kutokana na athari zake,” alisema Waziri Mitchell.

“Uingereza inafanya kazi kwa karibu na washiriki wa Afrika kupiga vita mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mifumo ya kukabiliana na madhara na kusaidia maisha ya walioathirika zaidi.”

Kuzinduliwa rasmi kwa miradi hii ya mabilioni kunaashiria kutimizwa kwa ahadi iliyotolewa na Waziri wa Uingereza anayesimamia Masuala ya Kigeni, James Cleverley, ‘uwekezaji wa dhati na wa kutegemewa barani Afrika’ alipozuru Kenya mnamo Disemba.

Ahadi hiyo pamoja na mikataba iliyoafikiwa katika Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) lililofanyika 2021 linaashiria nguvu ya ushirikiano kati ya Uingereza na bara la Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Kampuni iliyomshtaki Amadi kuhusu sakata ya dhahabu yahofia...

TUONGEE KIUME: Usichotakiwa kufanya ukiwa mwanamume usiye...

T L