• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:50 AM
Magari ya zimamoto yagongana kabla kuzinduliwa

Magari ya zimamoto yagongana kabla kuzinduliwa

NA ALEX KALAMA 

MAGARI mawili mapya ya zimamoto yaliyokuwa yanatoka jijini Mombasa ili kuzinduliwa rasmi kwenye sherehe ya ufunguzi wa kituo kipya cha idara ya zimamoto kilichojengwa mjini Kilifi, yaligongana katika eneo la Kwa Kadzengo katika barabara kuu ya Kilifi-Mombasa kabla hata hayajafika kwenye eneo la sherehe za uzinduzi huo.

Wahudumu wawili wa zimamoto walinusurika kifo. Kulingana na Waziri wa Barabara kaunti ya Kilifi Bi Cathrine Kenga, gari hilo liligonga ubavu wa gari jingine na kupoteza mwelekeo na kuyumba hadi kando ya barabara.

Waziri huyo hata hivyo amethibitisha kuwa dereva wa gari hilo yuko salama, huku mwenzake aliyekua naye akipata majeraha madogo na kukimbizwa katika hospitali ya Oasis eneo la Mtwapa.

Akizungumza na wanahabari mjini Kilifi, kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Kilifi Ibrahim Matumbo ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Watamu, ameitaka kamati ya bunge la kaunti kuhusu barabara kuwahoji waliohusika na ajali hiyo ili kutambua kiini halisi cha ajali hiyo.

Alilaumu idara ya barabara kwa kuajiri madereva wasiojimudu kiutendakazi.

“Naomba ile kamati ambayo inahusika na maswala ya barabara iweze kuangalia tena hawa watu kwa sababu mimi bado nafikiri wanahitaji kutuelezea ni kwa nini wamegongana wakati wote wametoka sehemu moja,” alisema Bw Matumbo.

Magari hayo ya zimamoto ambayo yalipaswa kuzinduliwa siku ya Jumatatu yalikuwa ni manne lakini kwa vile mawili yalipata ajali na kuharibika, Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alizindua mawili pekee ambayo yaligharimu jumla ya Sh125 milioni.

Akizungumzia muundo wa magari mawili ya zimamoto gavana Mung’aro alieleza kuwa wahudumu wote wa zimamoto watalazimika kufanyiwa upya mafunzo ya kazi hiyo chini ya usimamizi wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

“Wale wafanyakazi wote wa sekta ya zimamoto watapokea mafunzo upya na kuangalia uwezo kupitia kwa NYS, ndipo tuwaruhusu kuendelea kufanya kazi katika idara hiyo. Na wale ambao watafeli kupita baada ya mafunzo tutawaondoa wote kwa sababu hatutaki yale ambayo yametokea leo (jana Jumatatu) yajirudie tena,” alisema Bw Mung’aro.

Hata hivyo gavana huyo ameitaka idara ya maendeleo ya miji kujieleza zaidi baada ya vifaa vingine hitajika kukosekana kwa jengo hilo la kisasa lililogharimu serikali ya kaunti mamilioni ya pesa.

“Pia vilevile nitarudi kwenu idara ya maendeleo ili muniambie vizuri ni kwa nini vifaa vingine ambavyo ni hitajika vinakosekana katika jengo hili kwa sababu ukiangalia ofisi nyingine hata viti hakuna, meza hakuna… Nitahitaji kupata majibu ya hili ninalolisema,” alisema Bw Mung’aro.

  • Tags

You can share this post!

Lamu: Wanawake washikilia biashara ya matikitimaji...

AMINI USIAMINI: Utatozwa faini ya Sh40,000 ukimgusa Quokka

T L