• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 4:32 PM
Lamu: Wanawake washikilia biashara ya matikitimaji iliyowashinda wanaume

Lamu: Wanawake washikilia biashara ya matikitimaji iliyowashinda wanaume

NA KALUME KAZUNGU

MIAKA mitatu iliyopita, kisiwa cha Mkokoni katika Kaunti ya Lamu kilikuwa kikiongoza na kuvuma kwa ukuzaji wa tikitimaji.

Kisiwa hicho kinapatikana Lamu Mashariki, kikiwa karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Licha ya kutambulika kwa zao hilo, kisichojulikana na wengi ni kwamba hali ya anga katika kisiwa cha Mkokoni imekuwa ni ya hati hati kwani mvua haijakuwa ni yenye kutegemeeka kutosheleza zao la aina yoyote ile kila msimu.

Miaka nenda miaka rudi, kisiwa cha Mkokoni pia kimeshuhudia changamoto tele, ikiwemo wanyama pori na hali duni ya barabara, hali iliyowafanya wanaume pekee kumudu biashara ya kukuza matikitimaji kabla ya kuyatafutia soko maeneo ya mbali.

Kisiwa hicho ni makazi ya Waswahili wa jamii ya Wabajuni.

Katika miaka ya hivi punde, wanaume wameonekana kulemewa hadi kushindwa kabisa na kilimo na biashara ya matikitimaji.

Katika harakati za kuhifadhi hadhi ya kisiwa cha Mkokoni kama ngome ya kuzalisha matunda hayo aidha, wanawake wengi sasa wamejitosa kwenye ukulima wa zao hilo huku wakivuna pakubwa licha ya changamoto tele zilizopo.

Tima Abdulamin, mmoja wa wakulima wa matikitimaji kisiwani Mkokoni, alisema ili kumudu ugumu katika kukuza matikitimaji, wao kama wanawake waliafikia kubuni vyama vya ushirika kwa minajili ya kuendeleza kilimo hicho.

Tima Abdulamin, mmoja wa wakulima wa matikitimaji kisiwani Mkokoni ambaye hujitahidi na kuyauza katika mji wa kale wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kulingana na Bi Tima awali walikuwa wakijionea wanaume wakijifanyia ukulima binafsi, ambapo walijitolea kutayarisha mashamba, kuchota maji kutoka sehemu za mbali, ikiwemo kwenye mito na visima na kunyunyizia mimea yao tangia ingali midogo hadi kukomaa kwake sababu kuu ikiwa ni mvua kuadimika eneo hilo.

Kadhalika, wanaume walikuwa wakijitolea kushinda mashambani kulinda matikitimaji yao yasiharibiwe na wanyama pori, hasa nyani waliosheheni eneo hilo linalopakana na msitu mkuu wa Boni.

Mwishowe wanaume walichoka na kuamua kuupiga teke ukulima huo wa gharama si haba.

Kwa sasa wanaume waliojikita kwenye biashara ya matikitimaji wametorokea kwenye sekta ya uvuvi baharini.

Bi Abdulamin alisema ni maamuzi hayo ya wanaume kuacha ukulima wa matikitimaji ambapo yaliwasukuma kujitosa wazimawazima kwenye sektya hiyo.

Anasema hatua yao ya kujiunga katika vikundi imefaulisha pakubwa kilimo cha matikitimaji kwani wamekuwa wakivuna shehena kubwa kubwa kisiwani Mkokoni.

“Tulijua fika kuwa tukijifanyia kilimo cha kila mmoja kivyake hatungeweza kutokana na gharama zinazoambatana na ukuzaji wa matikitimaji. Ndiyo sababu tukaunda vyama vya ushirika, azma kuu ikiwa ni kuendeleza kilimo hicho kwetu Mkokoni. Twashukuru kwamba tumefaulu kupata mavuno si haba msimu huu,” akasema Bi Tima.

Bi Ruweida Mohammed ambaye ni mwanachama wa kikundi kimoja na Bi Abdulamin cha Mkokoni Women Empowerment Group, anasema wameweza kuajiri vibarua katika kuendeleza kilimo cha matikimaji.

Bi Mohammed anasema vibarua wao wamewagawanya kimajukumu. Kuna wale wa kupanda na kunyunyizia dawa na maji mimea.

Kuna wengine ambao kazi yao ni kufurusha wanyamapori mashambani na pia kuyatunza ili wezi wasipenye na kuiba mazao.

Matikitimaji kutoka kisiwa cha Mkokoni yakitandazwa kisiwani Lamu kuuzwa.
PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Mohammed pia alisema wameajiri wafanyakazi wa kuvuna na kusafirisha matikitimaji yao kutoka mashambani hadi mjini kabla ya wao wenyewe kuanza kutafuta mbinu za kusafirisha matunda yao hadi kufikia soko.

“Ingekuwa ni sisi wenyewe tunajifanyia kazi hizo zote kama walivyokuwa wakifanya wenzetu wanaume hatungeweza. Tumeekeza kwenye vyama vyetu vya ushirika, ambapo kuna fedha tumetenga kuwalipa wafanyakazi wanaotusaidia kukuza matikitimaji hadi yafikie kiwango cha kuvunwa na kufikia soko. Ukulima wa matunda haya ni ghali hasa huku kwrtu Mkokoni lakini hatufi moyo. Tunagharimika lakini biashara nayo inalipa,” akasema Bi Mohammed

Akina mama hao aidha wanaisihi serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuwasaidia, hasa kiusafiri wakitaja kuwa kusafirisha na kufikisha shehena moja ya matikitimaji kutoka kisiwa cha Mkokoni hadi kisiwa cha Lamu au jeti ya Mokowe ni ghali.

“Kusafirisha shehena ya matikitimaji kutoka Mkokoni hadi maeneo kama vile mji wa kale wa Lamu au jeti ya Mokowe utahitajika kulipa hadi Sh60,000 kwa boti ya kibinafsi. Mara nyingine tunalazimika kuruhusu wenye maboti kupandiza abiria ili angalau tulipe kiwango wastani kidogo ambacho ni Sh45,000. Changamoto ni kwamba matunda yetu huharibika kwa kukanyagwa botini na walioabiri chombo. Pia kudundishwadundishwa kwa matikitimaji na boti husababisha mengi kufikishwa sokoni yakiwa yakiwa yameharibika,” akasema Bi Amina Ali, mmoja wa wakulima wa matikitimaji.

Waliiomba serikali kuu kuwasaidia kuijenga na kuifungua rasmi barabara ya umbali wa zaidi ya kilomita 250 kutoka Mkokoni hadi Kiunga na kisha kuunganisha Kiunga na Msitu wa Boni hadi Hindi, Lamu Magharibi.

Kwa miaka mingi barabara hiyo haijakuwa ikitumiwa na wakazi kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Bi Salma Aboud anasema endapo usafiri wa barabara unaounganisha Lamu Mashariki na Lamu Magharibi utafunguliwa utaleta afueni kwa wakulima na pia wakazi wenyewe.

“Ukitazama usafiri wa barabara ni rahisi ukilinganisha na ule wa baharini. Badala ya kulipa karibu Sh60,000 kusafirisha shehena moja ya matikitimaji kutoka Mkokoni hadi Lamu kupitia njia ya bahari, watufungulie barabara yetu ambapo tutalipa kati ya Sh10,000 na Sh15,000 pekee kusafirisha mizigo hiyo,” akasema Bi Aboud.

Hussein Mahir, mkazi wa kisiwa cha Lamu aliwapongeza akina mama wa Mkokoni kwa juhudi zao katika kuendeleza kilimo cha matikitimaji licha ya changamoto zilizoko.

Bw Mahir aliiomba serikali ya kaunti ya Lamu kupitia kwa gavana, Issa Timamy kujenga kiwanda cha matunda kitakachowaletea wakulima wa matikitimaji soko la karibu na wazi.

“Nawashukuru hawa wanawake wetu wa kutoka kisiwa cha Mkokoni. Ugumu uliopo katika kukuza na kuendeleza kilimo cha matikitimaji yamkini ulishinda hata sisi wanaume. Akina mama wana bidii na wastahili kupigwa jeki kuendeleza kilimo hicho. Ndio sababu ninamsihi gavana wetu, Issa Timamy na serikali ya kitaifa kwa jumla kusikia kilio cha hawa wamama wetu na kuwasaidia kuboresha miundomsingi, hasa usafiri ili iwe rahisi kwao kuendeleza kilimo cha matikitimaji,” akasema Bw Mahir.

  • Tags

You can share this post!

Vuguvugu la Operation Linda Ugatuzi laitaka ICC...

Magari ya zimamoto yagongana kabla kuzinduliwa

T L