• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Mahakama yaelezwa jinsi wasichana wadogo walivyonajisiwa kisha wakauawa

Mahakama yaelezwa jinsi wasichana wadogo walivyonajisiwa kisha wakauawa

NA TITUS OMINDE

MAHAKAMA Kuu ya Eldoret mnamo Jumanne iliambiwa Juma Wanjala Evans aliyekiri kutekeleza mauaji, alimnajisi na kumnyonga mmoja wa watoto watano ambao alidaiwa kuwaua miaka minne iliyopita katika mji wa Moi’s Bridge, Kaunti ya Uasin Gishu.

Alipokuwa akitoa ushahidi mbele ya jaji Reuben Nyakundi, mamake mmoja wa watoto hao Bi Sharon Sakwa alisimulia mahakamani jinsi alivyoshtuka mwili wa bintiye wa umri wa miaka saba ulipogunduliwa kando ya reli katika eneo la Soweto, Moi’s Bridge.

Bi Sakwa aliambia mahakama kuwa hali ya mwili huo ilionyesha wazi kuwa mtoto huyo alinajisiwa kabla ya kunyongwa na mtesaji wake.

“Jioni ya saa kumi na mbili mnamo Desemba 31, 2019, nilimtuma binti yangu kwa duka la karibu na nilipoona anakawia kurudi nyumbani niliingiwa na wasiwasi na kuanza kumtafuta binti yangu bila mafanikio. Asubuhi iliyofuata mwili wake uliokuwa umekatwakatwa uligunduliwa kando ya njia ya reli ukiwa na dalili za unajisi na kunyongwa,” Bi Sakwa aliambia mahakama huku akibubujikwa na machozi.

Bi Sakwa alikuwa ameripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Moi’s Bridge siku iliyotangulia.

Alipokamatwa Julai 17, 2017, Wanjala alikiri kuwaua wasichana watano baada ya kuwashambulia na kuwanajisi.

Kulingana na taarifa yake iliyopo mahakamani, Wanjala alifichua kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwamba alitekeleza mauaji hayo kati ya Desemba 31, 2019, na Juni 15, 2021.

Alinajisi waathiriwa wake kabla ya kuwanyonga hadi kufa.

Katika ungamo la kutisha lililotolewa kwa wapelelezi wakati wa kuigiza upya jinsi alivyotekeleza misheni yake ya kikatili, mshukiwa huyo alieleza kwa kina jinsi alivyokatiza maisha ya watoto watano baada ya kuwanajisi.

Wakati wa uchunguzi pia aliongoza wapelelezi kwenye maeneo ya kila mauaji, ambapo mabaki ya watoto waliouawa yalipatikana.

“Katika kisa kimoja kama hicho, mwili ulioharibika wa mtoto uligunduliwa mnamo Juni 15, 2021, karibu na Bwawa la Baharini, baada ya kutoweka kwa zaidi ya wiki moja.

Miili yote mitano ilikuwa na dalili zinazofanana za kunyongwa, kunajisiwa, na majeraha ya kimwili yaliyoonekana.

Tayari mashahidi wanne wametoa ushahidi katika kesi hiyo ambapo Wanjala anadaiwa kumuua Stacy Achieng Nabiso.

Maelezo ya nakala za mashtaka yanasema kwamba usiku wa Desemba 31, 2019, na Januari 1, 2020, katika eneo la Soweto ndani ya mji wa Moi’s Bridge ndani ya kaunti ndogo ya Soy alimuua Stacy Achieng Nabiso.

Mashahidi watano waliosalia wanatarajiwa kutoa ushahidi tarehe 21 Novemba kesi itakapoendelea.

  • Tags

You can share this post!

Madereva wa masafa marefu wahamasishana, waombea nafsi za...

Bloga ashtakiwa kwa kuchapisha habari za uongo kuhusu Naibu...

T L