• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Madereva wa masafa marefu wahamasishana, waombea nafsi za wenzao walioangamia ajalini

Madereva wa masafa marefu wahamasishana, waombea nafsi za wenzao walioangamia ajalini

NA FRIDAH OKACHI

CHAMA cha madereva wa masafa marefu nchini, kimefanya maombi maalum eneo la Maili Tisa mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu kuombea nafsi za wenzao waliopoteza maisha yao kwenye ajali za barabarani.

Walitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha zaidi madereva kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za barabarani.

Madereva hao walihimizwa kuwa makini wanapoendesha magari hayo ili kupunguza visa vya ajali na kuimarisha usalama barabarani.

Paul Kipchumba kutoka ofisi ya Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu aliwataka madereva kuendesha magari kwa uangalifu.

Vile vile, aliwasihi madereva kuacha mzaha wa kupokea simu na kuzungumza wakati wanaendesha magari.

Afisa huyo alitaja kuwa madereva wengi hawapati muda wa kutosha wa kupumzika, jambo ambalo huchangia ajali barabarani.

Aidha mwenyekiti wa muungano wa madereva wa malori ya trela Nicholus Mutua, amewashauri madereva hao kutotumia simu na kutafuta muda wa mapumziko kabla na baada ya safari.

Wengi wa madereva wamekuwa wakiendesha magari kwa saa 10 mfululizo bila kupunzika.

Roman Waema, ambaye ni miongoni mwa madereva waliohudhuria mkutano huo, ameomba kaunti ya Uasin Gishu kuwajengea vyumba vya mapumziko na kuongezwa kwa taa katika eneo hilo la Maili Tisa ili kuimarisha usalama.

Eneo la Maili Saba limekuwa likitajwa kuwa hatari kutokana na ajali ambazo hutokea mara kwa mara.

  • Tags

You can share this post!

Walimu wataka Kilifi iorodheshwe kuwa mazingira magumu ya...

Mahakama yaelezwa jinsi wasichana wadogo walivyonajisiwa...

T L