• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Mahakama yaokoa spika katika meno ya madiwani

Mahakama yaokoa spika katika meno ya madiwani

Na PHILIP MUYANGA

BUNGE la Kaunti ya Tana River limezimwa kutekeleza azimio lililopitishwa la kumuondoa ofisini Spika Michael Nkaduda.

Mahakama ya Leba pia iliagiza bunge hilo kutochapisha au kutangaza nafasi ya spika kuwa wazi au kuijaza.

Jaji Byram Ongaya aliamua kwamba bunge hilo lilikiuka kanuni kwa kuanzisha mchakato wa kumuondoa ofisini Spika Nkaduda.

Jaji huyo alisema mswada wa kumtimua Bw Nkaduda haukutimiza lengo la kumuondoa ofisini kulingana na sheria ya serikali za kaunti kwa kuwa haikuwa umeungwa na thuluthi moja ya madiwani wa bunge hilo la kaunti.

“Vilevile, mahakama imebaini kwamba alivyoeleza mlalamishi, mswada wa kumuondoa ofisini ukidai kuorodhesha sababu, haukutaja sababu, jinsi inavyohitajika katika sheria hiyo,” alisema Jaji Ongaya.

Mahakama ilisema kwamba ilipata kuwa kamati iliyopendekeza atimuliwe haikumpa Bw Nkaduda muda wa kujieleza kikamilifu.

“Hii ilikuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki ya mlalamishi ya kujitetea. Hakuna aliyepinga kuwa mlalamishi alikuwa mgonjwa ilivyodhihirishwa kwa kamati ya mawakili wake,” alisema Jaji Ongaya.

Jaji Ongaya pia alisema kutimuliwa kwa spika huyo kulifanywa kwa kupuuza haki yake ya kujitetea kwa hivyo mchakato wote ulikuwa na dosari.

Bw Nkaduda alikuwa amelalamika kuwa mchakato haukusimamiwa na diwani aliyechaguliwa kwa mujibu wa sehemu 9(4) ya Sheria ya Serikali za Kaunti na hatua ya kamati ya kuwasilisha ripoti kwa bunge la kaunti ilikuwa kudharau mahakama na ilikiuka sheria.

Spika huyo alishtaki bunge la Kaunti, karani wa bunge hilo na madiwani watatu pia wa bunge hilo.

Alisema bunge la Kaunti, likifahamu kuwa mapendekezo yake yakitekelezwa yangefanya aondolewe kutoka ofisi ya umma, halikumpa ilani kumweleza aina na sababu za kuchukuliwa hatua ya nidhamu dhidi yake.

Bw Nkaduda alisema kwamba kamati ya bunge la kaunti ilikuwa njama iliyopangwa kumtimua kutoka ofisini bila kufuatia mchakato unaostahili kisheria.

Kwa upande wake, bunge la kaunti lilisema kwamba lilimsikiliza aliyewasilisha mswada wa kumtimua na baada ya kufanya uchunguzi likampata spika na hatia ya kukosa nidhamu ilivyoelezwa.

Bunge hilo la kaunti lilisema kwamba lilijadili mswada wa kumuondoa ofisini kwa kuzingatia ripoti ya kamati.

Jaji Ongaya alihimiza pande zote kupatana na kuwasilisha makubaliano kortini kesi itakapotajwa au zichukue hatua kuhakikisha imekamilishwa haraka.

You can share this post!

Serikali imeshindwa kukabili ukame – Ripoti

Huzuni tele ajuza waliouawa kwa madai ya uchawi wakizikwa

T L