• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:55 AM
Serikali imeshindwa kukabili ukame – Ripoti

Serikali imeshindwa kukabili ukame – Ripoti

Na SILAS APOLLO

SERIKALI imefeli kudhibiti majanga kama vile ukame licha ya kuelekeza mabilioni ya fedha katika mipango ya kupambana na makali yake, ripoti mpya imeonyesha.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu ilisema licha ya Sh25 bilioni kutumika katika mipango ya kupambana na ukame tangu 2015, janga hilo bado linasababisha vifo na uharibifu wa mali.

Ukame ambao sasa unashuhudiwa katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya umesalia kuwa chanzo cha changamoto zinazowasibu wakazi katika maeneo hayo.

Kufikia sasa, jumla ya kaunti 23 nchini zinaathiriwa na makali ya ukame na ambako wakazi wanahitaji msaada wa chakula na lishe kwa mifugo.

Miongoni mwa kaunti hizo ni: Baringo, Kajiado, Kwale, Laikipia, Lamu, Makueni, Meru, Taita Taveta, Tharaka Nithi na Pokot Magharibi.

Nazo nyingine ni; Garissa, Isiolo, Kitui, Mandera, Marsabit, Samburu, Turkana, Tana River na Wajir huku kaunti za Narok, Embu na Nyeri zikikabiliwa na hatari ndogo ya kuathirika na ukame.

Katika ripoti hiyo kuhusu juhudi za kudhibiti ukame nchini kati ya 2015 na 2020, Bi Gathungu anasema hakujakuwa na ushirikishi mwafaka kati ya Serikali Kuu na serikali za kaunti katika mchakato huo.]

“Vile vile, hakujakuwa na ushirikiano mzuri kati ya ngazi hizi za serikali na mashirika yasiyokuwa ya serikali katika vita dhidi ya makali ya ukame,” anaeleza katika ripoti hiyo.

“Kwa hivyo, kushindwa kwa serikali katika kushughulikia mapungufu haya kumefanya hali kuwa mbaya zaidi,” Bi Gathungu anaongeza.

Serikali, kulingana na ripoti hiyo, kwa miaka mingi imefeli kutunga sheria na sera za kuimarisha mpango wa kukabiliana na ukame.

“Vile vile, serikali imefeli kushirikisha jamii athirika katika jitihada za kusaka suluhu la kudumu kwa changamoto hili na kufanya hali kuwa mbaya zaidi,” ripoti hiyo inaongeza.

Hii ndio maana jamii katika maeneo yaliyoathirika zaidi hayajapata afueni licha miradi mingine iliyoanzishwa kudhibiti hali hiyo.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya miradi hiyo kama vile ujenzi wa mabwawa na visima, haijakamilika au imefeli kuanzishwa kutokana na ufisadi na utepetevu miongoni mwa maafisa wa serikali. Baadhi ya miradi ilisambaratika kutokana wizi wa fedha zilizotengwa kuifanikisha,” ripoti hiyo inaongeza.

Uchunguzi huo uliendeshwa kufuatia malalamishi kutoka kwa umma kuhusu jinsi serikali inavyoshughulikia janga la ukame.

Malalamishi hayo yaliwasilishwa kupitia bungeni na ripoti mbalimbali katika vyombo vya habari.

You can share this post!

Kinara wa KNUT amrukia Sossion kuhusu zogo

Mahakama yaokoa spika katika meno ya madiwani

T L