• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Makatibu: Spika Wetang’ula akunja mkia na kusitisha upigaji msasa Bungeni

Makatibu: Spika Wetang’ula akunja mkia na kusitisha upigaji msasa Bungeni

NA CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesitisha shughuli ya usaili wa makatibu wa wizara kufuatia agizo la Mahakama ya Leba na Masuala ya Uajiri lililotolewa Novemba 15, 2022.

Kwenye taarifa kwa Kamati za Bunge zilizokuwa zikiendesha shughuli hiyo katika majengo ya Bunge, Nairobi, Bw Wetang’ula ameagiza kwamba usaili huo usimamishwe hadi mawakili wa bunge watakapofaulu kubatilisha uamuzi huo uliotolewa na Jaji Nzioka wa Makau.

“Shughuli ya usaili wa watu waliopendekezwa kuhudumu kama Makatibu wa Idara za Wizara za Serikali imesitishwa hadi agizo lingine litakapotolewa kuhusu suala hili. Kamati ambazo zilikuwa zimekamilisha shughuli hiyo zinaagizwa kusitisha shughuli zozote kuhusu suala hilo kama vile utayarishaji wa ripoti na uwasilishaji ripoti hiyo kwenye kikao cha bunge lote, hadi mwelekeo utakapotolewa baadaye, Bw Wetang’ula akasema.

“Vikao vya usaili wa makatibu wateule vitaendelea baada ya mahakama kutoa agizo,” akaongeza.

Mnamo Jumanne, Jaji Makau alisitisha shughuli hiyo ya usaili wa makatibu hao wateule 51 waliopendekezwa na Rais William Ruto.

Hii ni baada ya Chama cha Mawakili Nchini (LSK) kuwasilisha kesi mahakamani kikisema uteuzi wa watu hao haukuafiki hitaji la kikatiba la usawa wa kijinsia, kimaeneo na kikabila. Chama hicho kilisema uteuzi huo haukufanywa kwa njia inayofanya Wakenya wote kuhisi kuhusishwa.

“Aidha, orodha ya watu hao 51 waliopendekezwa kuwa makatibu wa idara za wizara za serikali haikuwa na wawakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu, watu kutoka jamii zilizotengwa, wakongwe miongoni mwa makundi mengine ya wanajamii,” LSK ikasema katika kesi yake.

Shughuli ya usaili au kupigwa msasa kwa Makatibu hao wateule ilianza Jumatatu, Novemba 14, 2022. Na kufikia Jumatano, shughuli hiyo ilipositishwa jumla ya makatibu 24 wateule walikuwa wamepigwa msasa.

Miongoni mwao ni Chris Kiptoo (Wizara ya Fedha), Dkt Korir Sang’oei (Katibu wa Masuala ya Kigeni) na Patrick Mariru (Katiba katika Wizara ya Ulinzi).

You can share this post!

Magenge yakaidi Kindiki, yaendelea kupora wakazi

Makatibu wa Kenyatta kuendelea kuhudumu wale wa Ruto...

T L