• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Malala akemea wabunge Magharibi kutumia michango ya shule kujikweza kisiasa

Malala akemea wabunge Magharibi kutumia michango ya shule kujikweza kisiasa

NA JESSE CHENGE

KATIBU Mkuu wa chama cha UDA, Cleophas Malala, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kundi la wabunge wa Magharibi mwa Kenya anaohoji wanahadaa watu wa eneo hilo kupitia michango ya miradi ya maendeleo kukweza umaarufu wao kisiasa.

Bw Malala anasema wabunge hao (ingawa hajaweka paruwanja orodha ya majina yao), wanatumia jukwaa la harambee za ujenzi wa shule kusaka umaarufu kisiasa katika jamii ya Waluhya.

Akielezea kutoridhishwa kwake na hatua hiyo, Katibu Mkuu huyo amesema badala ya kuzindua kampeni za mapema wanapaswa kuhudumia wananchi waliowachagua.

Maarufu kama Kundi la Wabunge wa Eneo la Magharibi, Malala amesema ni vuguvugu la ‘wanasiasa matapeli’ ambalo wenyeji wanapaswa kuwa makini nalo.

“Linadanganya watu wa Magharibi mwa Kenya kupitia ‘’miradi’ ya harambee za shule kutafuta umaarufu. Isitoshe, wanatumia jukwaa ya michango kudai wanaleta umoja wa jamii. Huo ni utapeli wa kisiasa,” akadai, akiwataka kukoma kampeni za mapema.

Bw Malala alisema, viongozi na wanasiasa wa jamii ya Waluhya kwa sasa wanalenga siasa za kitaifa ila si za eneo hasa kutokana na baadhi ya nyadhifaa kuu serikalini wanazoshikilia.

“Umoja na maendeleo ya kitaifa ndio tunapaswa kuangazia,” alisisitiza, akihimiza viongozi kutoka Magharibi mwa Kenya kucheza mahesabu ya siasa za kitaifa.

Alisema umoja wa jamii na kujiweka kwenye hadhi ya kitaifa ndio utasaidia eneo hilo kupata maendeleo.

Tangu kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala cha UDA, Malala amekuwa akihimiza na kuvitaka vyama tanzu Kenya Kwanza kuvunja vyama vyao na kuunda muungano wenye sura ya kitaifa.

Aidha, amekuwa akipigia upatu kunenepeshwa kwa chama cha UDA.

Huku chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto kikijiandaa kufanya chaguzi za chama mashinani Desemba 202, Bw Malala amesihi Ford Kenya (chake Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula) na ANC – Chama cha Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi kuungana chini ya UDA kwa ajili ya umoja na maendeleo.

Akizungumza Mjini Bungoma, ambapo alikaribisha wanachama waliohama vyama vingine kujiunga na UDA, Malala alisema kwamba siasa za kuunganisha jamii ya Waluhya ni za zamani, na sasa ni jukumu la viongozi wa Magharibi mwa Kenya kuyapa kipaumbele maendeleo ya Wakenya kupitia UDA.

“UDA imejiandaa vizuri kwa chaguzi zijazo za chama,” alisema Malala.

Aidha, alihimiza viongozi wa eneo la Magharibi kuungana chini ya UDA na kuweka maendeleo ya Kenya mbele.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi eneo la Kwasasi-Ingini lilivyopata jina jipya la...

Leo ni siku ambayo Rais Ruto aliahidi kukutana na Museveni...

T L