• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Jinsi eneo la Kwasasi-Ingini lilivyopata jina jipya la ‘Magogoni’

Jinsi eneo la Kwasasi-Ingini lilivyopata jina jipya la ‘Magogoni’

NA KALUME KAZUNGU

SIFA za kijiji cha Magogoni, Kaunti ya Lamu zilianza kuenea miaka ya sabini (1970s).

Ni kijiji ambacho kimeshuhudia maendeleo si haba kadri miaka inavyosonga.

Kijiji hicho kwa sasa kinajivunia kuwa mwenyeji wa kambi ya pili kubwa zaidi ya jeshi la wanamaji (nevi) nchini baada ya ile ya Mtongwe iliyoko katika Kaunti ya Mombasa.

Licha ya kubeba hadhi hiyo kubwa, wenyeji wa kijiji cha Magogoni bado wanaishi kiskwota kwani kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50 ya uhuru, hakuna mkazi hata mmoja ambaye amekabidhiwa hatimiliki ya ardhi.

Hali hiyo imewasukuma wakazi kuishi kwa hofu bila kufahamu ni lipi litawakumba katika siku za usoni, hasa kuhusiana na ardhi zao kwani hakuna stakabadhi yoyote inayowatambulisha wao kuwa wamiliki halisi wa ardhi zilizoko Magogoni.

Taifa Leo ilizama chini kuchambua ni nini hasa kilichosukuma kitongoji cha Magogoni kubandikwa jina hilo.

Je, kwa nini wakazi wa Magogoni kusalia maskwota miaka yote hiyo licha ya kuwa waanzilishi wa kiambo hicho ambacho ni mwenyeji wa kambi ya haiba kubwa ya nevi Lamu na nchini kwa ujumla?

Mwanahistoria na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu Mohamed Mbwana anasema kijiji cha Magogoni kilizinduliwa na wakimbizi wa kwanza wa ndani kwa ndani nchini (IDP) wa asili ya Kibajuni.

Wakimbizi hao walikuwa wamefurushwa na wapiganaji walioendeleza vita vya Shifta kutoka kwenye vijiji vyao eneo la Kiunga lililoko mpakani mwa Kenya na Somalia miaka ya sitini (1960s).

Kulingana na Bw Mbwana, pindi Wabajuni walipokusanya virago kutoka Kiunga, walihamia kisiwa cha Manda kilichoko Lamu Magharibi ambako waliishi kwa muda.

Ikumbukwe kuwa kitega uchumi kikuu na cha asili cha jamii ya Wabajuni kilikuwa ni kilimo.

Katika kisiwa cha Manda, ukulima haungefaulu kutekelezwa vyema kwani ardhi eneo hilo ilisheheni changarawe na mawe ilhali ikikosa rutuba.

Ni kutokana na hali hiyo ambapo wazee Wabajuni waliafikia kuvuka eneo la karibu liitwalo Kwasasi-Ingini ili kuwawezesha kuendeleza kilimo kati ya 1970 na 1978.

Eneo hilo la Kwasasi-Ingini lilikuwa limesheheni msitu wenye miti mikubwa.

Mja aliyekuwa na nia ya kutengeneza shamba la kilimo au makazi hakuwa na budi ila kuufyeka msitu, ikiwemo kuangusha miti hiyo minene na yenye magogo makubwa makubwa.

Gogo, kulingana na maelezo ya kimsingi ya kamusi, ni kipande kikubwa na kinene cha mti ulioanguka au kukatwa.

Maskwota wa kijiji cha Magogoni, kaunti ya Lamu wakijitokeza kutazama nyumba zao zilizoharibiwa wakati walipozozana na mmoja wa mabwanyenye kuhusu umiliki wa ardhi eneo hilo. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hatua ya wazee Wabajuni kuvamia eneo la Kwasasi-Ingini na kufyeka msitu, ikiwemo kuangusha miti minene ili kujipatia shamba la shughuli za kilimo iliacha magogo mengi yakitapakaa kila mahali.

Ni kutokana na mandhari hayo ambapo eneo la Kwasasi-Ingini lilibandikwa jina jipya la ‘Magogoni’.

Isitoshe, msitu wa Kwasasi-Ingini ulitambulika kwa kuhifadhi nyoka wakubwa aina ya chatu ambao walikuwa na uzito ulioshabihiana na gogo.

Kwa mintarafu hiyo, eneo hilo pia lilijipatia umaarufu wa kuwa na magogo ya chatu, hivyo kuitwa ‘Magogoni’.

Mnamo miaka ya tisini (1990s), afisa wa jeshi la nevi na mwenye asili ya Kibajuni kutoka kisiwa cha Siyu kwa jina Abdallah Rafurafu aliwasili katika eneo hilo la Magogoni, ambapo aliwarai wazee Wabajuni kumsaidia kupata pahala pa kuishi.

“Bw Rafurafu alikuwa akiaminiwa na jamii yetu ya Kibajuni kwani tulimchukulia kuwa mmoja wetu. Alikuwa akiisaidia jamii kwa misaada mbalimbali wakati akihudumia jeshi la nevi la Kenya. Alipowasihi wazee kumpa ardhi ya kuishi walikubali mara moja, hivyo kumkatia sehemu kubwa ya shamba ili naye amiliki kipande cha ardhi kama Wabajuni wenzake,” akasema Bw Mbwana.

Ingawa hivyo, inaelezwa kuwa masaibu ya jamii ya Wabajuni wa Magogoni yalizidi baadaye pale Bw Rafurafu alipoenda kinyume na maagano na kuuza shamba alilopewa kwa serikali ya Kenya kwa minajili ya ujenzi wa kambi ya sasa ya nevi.

Bi Arafa Lacho Bashora,46, ambaye ndiye mzee wa kijiji cha Magogoni, anasema jamii iliachwa na mshangao miaka michache baadaye kwani serikali iligeuka na kuanza kuwafurusha watu kwa lazima kutoka kwa makazi yao kupisha ujenzi wa kambi ya jeshi la wanamaji.

Bi Arafa Lacho Bashora akionyesha stakabadhi zinazoonyesha majina ya wakazi ambao wamekuwa wakiishi eneo la Magogoni kwa muda mrefu. Wakazi wanaililia serikali kuwapa hatimiliki za ardhi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ujenzi wa kambi hiyo ulianzishwa 1992, ambapo kufikia 1995 ulikuwa umekamilika na kupewa utambulisho rasmi kuwa kambi ya nevi ya Kenya iliyoko Lamu.

Bi Lacho ni mama na pia nyanya, akiwa na wajukuu zaidi ya watano, wote wakiwa wamezaliwa, kulelewa na hata kuolewa katika kijiji hicho cha Magogoni.

“Babangu ni miongoni mwa walioanzisha kijiji chetu cha Magogoni. Kaburi lake liko pale ndani ya kambi ya nevi. Twasikitika kwamba hiari ya wazazi wetu kutoa ardhi na kumkabidhi mtu waliyemchukulia kuwa mmoja wao iligeuka baadaye na kuwa karaha kwao. Tulifurushwa kutoka kwa ardhi zetu kwa lazima bila kufidiwa. Hapa tulipo leo japo ni Magogoni lakini kitovu halisi cha kitongoji chetu ni pale ambapo kambi ya nevi imejengwa,” akasema Bi Lacho.

Kijiji cha sasa cha Magogoni ambapo watu wanaishi kiko karibu mita 300 kutoka kwenye kambi ya nevi.

Kufikia sasa, kijiji hicho kimehifadhi karibu familia 400 zinazojumuisha karibu makabila yote zaidi ya 40 ya Kenya.

Cha kusikitisha ni kwamba hakuna hata familia au mkazi mmoja anayemiliki hatimiliki hadi sasa.

“Nimezaliwa na kukulia hapa tangu udogoni hadi sasa ambapo mimi ni nyanya. Kinachonisikitisha ni kwamba bado sijapata hatimiliki ya ardhi hapa. Twaiomba serikali kutuonea imani sisi waanzilishi wa kijiji cha Magogoni. Watugawanyie hizi ardhi na kutupa hatimiliki ili tujiendeleze,” akasema Bi Lacho.

Naye Bw Ali Keah, ambaye ni mmoja wa wazee wa kijiji cha Magogoni, anasikitika akisema kwamba licha ya kuishi eneo hilo kwa miongo kadhaa sasa, serikali bado inaendelea kuwatelekeza na hata kuwaacha wakihangaishwa kila kukicha na mabwanyenye wanaozilenga ardhi hizo.

Magogoni ni eneo linalokaribiana na mradi wa bandari ya Lamu na Miundomsingi ya Uchukuzi wa Kenya, Ethiopia na Kusini mwa Sudan (Lapsset).

Bw Keah anasema ukosefu wa hatimiliki za ardhi za Magogoni umezuia maendeleo mengi kutekelezwa kwani wengi wao wanahofia kujiendeleza wakijua fika kuwa huenda wakafurushwa wakati wowote sawa na ilivyofanyikia enzi za akina babu wao.

Anasema vipande vya ardhi vya Magogoni mara nyingi vimekuwa vikilengwa na mabwanyenye.

“Hao mabwanyeye wanatusumbua na kutuhangaisha sana hapa. Wanang’ang’ania kupata kipande cha ardhi Magogoni, iwe ni kwa kheri au kwa shari kutokana na kwamba eneo hili limekaribiana na mradi huo mkubwa wa Lapsset. Twaomba serikali kuu, kaunti na Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) kutufikiria sisi wakazi wa Magogoni. Tugawiwe hizi ardhi na kupewa hatimiliki ili tuwe huru kujiendeleza,” akasema Bw Keah.

  • Tags

You can share this post!

Wapenzi watatu wa mwanamke aliyetoweka wazungumza

Malala akemea wabunge Magharibi kutumia michango ya shule...

T L