• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Malala haoni boriti katika jicho lake ila kwa mwingine

Malala haoni boriti katika jicho lake ila kwa mwingine

Na CHARLES WASONGA

TANGU wiki jana, wanasiasa kutoka maeneo ya Magharibi, Rift Valley na Pwani wamekuwa wakimsuta kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kutumia handisheki kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kufaidi eneo la Luo Nyanza anakotoka.

Wanasiasa kutoka Magharibi ndio wametumia muda wao mwingi kumkaripia Odinga, wakidai ametelekeza eneo hilo ilhali wakazi wamekuwa wakimuunga mkono kisiasa tangu 1997 alipowania urais kwa mara ya kwanza.

Wakiongozwa na Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala, na mbunge wa Lugari, Ayub Savula, walidai kwamba licha ya jamii ya Waluhya kumpa Odinga kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa 2017, amewasahau na sasa anapeleka maendeleo Luo Nyanza pekee.

Wanasiasa hawa walikuwa wakirejelea ziara ya hivi majuzi ya Rais Kenyatta katika kaunti za Kisumu na Siaya ambapo alizindua miradi kadha ya maendeleo.Kilele cha ziara hiyo ilikuwa Juni mosi ambapo kiongozi wa taifa aliongoza sherehe za 58 za Sikukuu ya Madaraka Dei katika uwanja mpya wa michezo wa Jomo Kenyatta.

Kwa mtazamo wangu, lalama za Malala na wenzake hazina mashiko hata kidogo. Ziara ya Rais ilipangwa na Ikulu, nayo miradi aliyozindua Kisumu na Siaya ilifadhiliwa na serikali kuu.Ngazi hii ya serikali inaongozwa na Rais Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa Kitaifa na Serikali Kuu wala sio Odinga.

Hivyo, jambo la busara ni kwa wanasiasa hawa kuelekeza malalamishi yao kwa Rais Kenyatta sio Odinga.Pili, miradi kama vile Bandari ya Kisumu, ukarabati wa reli kutoka Naivasha hadi Kisumu na Kisumu hadi Butere, itasaidia eneo zima la Magharibi si Luo Nyanza pekee.

Kimsingi, kwa kuwa kaunti za Kisumu na Siaya zinapakana na kaunti za Vihiga na Kakamega, kuna muingiliano mkubwa kati ya wakazi wa kaunti hizi nne katika nyanja zote za maisha. Ina maana kuwa, kwa mfano, mradi wa maji uliozinduliwa mjini Yala, Kaunti ya Siaya, pia utafaidi wakazi wa kaunti jirani za Kakamega na Vihiga.

Tatu, ni kinaya kwamba huku Malala na wenzake wakimlaumu Odinga kwa “kutoleta miradi kwetu Kakamega”; yeye pia amelaumiwa pakubwa kwa kuhujumu mpango wa bwanyenye Narendra Raval kufufua kiwanda cha sukari cha Mumias.Hii ndio maana juzi alirushiwa cheche katika hafla fulani ya mazishi Kakamega, wakazi na viongozi wa mashinani wakimsuta kwa kuvuruga juhudi za kufufua kiwanda hicho.

Cheche hizo zilitokana na madai kuwa Malala na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi, walisisitiza bwwanyenye huyo anayemiliki kampuni ya vyuma ya Devki Group sharti “ashauriane nasi kama viongozi kabla kutwaa usimamizi wa Mumias”.Viongozi wa Magharibi wanafaa kuelewa kuwa siasa kama hizi ndizo hufifisha maendeleo eneo lao wala sio handisheki ya Kenyatta na Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Mama mpiganaji wa Mau Mau aeleza dhuluma walizopitia

FAUSTINE NGILA: Hatua ya Nigeria kuzima Twitter itaumiza...