• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
Mama mpiganaji wa Mau Mau aeleza dhuluma walizopitia

Mama mpiganaji wa Mau Mau aeleza dhuluma walizopitia

Na SAMMY WAWERU

GRACE Njoki Mwangi ni mama mchangamfu na mkarimu, hulka ambazo zitakuvutia unapotangamana naye.

Alikuwa miongoni mwa majasusi wa MauMau, na baadaye kujiunga nao katika Msitu wa Tumutumu, ulioko eneo la Mathira, Kaunti ya Nyeri, alipoanza kuandamwa na askari wa mkoloni ilipobainika alishirikiana na vuguvugu hilo.

Oparesheni ya kukomboa Kenya kutoka kwa minyororo ya Uingereza, aliingilia akiwa chini ya umri wa miaka 15.Wiki iliyopita, Juni 1, 2021 Kenya iliadhimisha miaka 58 ya uhuru wa kujitawala, na licha ya umri wa nyanya huyu kusonga ni mwepesi wa kukumbuka mahangaiko aliyopitia, pamoja na wenzake.

Hutembea kwa kutumia mkongojo, kutokana na jeraha baya alilouguza wakati akiokoa maisha yake.Mwaka wa 1952, Njoki maarufu kama Cucu Kanguniu, pamoja na marafiki wake walikamatwa. Aidha, walisalia kizuizini muda wa wiki moja.

Walitakiwa kufichua siri za majenerali wa vita vya MauMau na ‘wanajeshi’ wao (vilivyotekelezwa kati ya 1951 – 1957), waliokuwa katika msitu wa Tumutumu, Aberdare, Mlima Kenya, kati ya misitu mingineyo.

Njoki hata hivyo hakuwa radhi kutoboa siri. Alikuwa amekula kiapo, na lazima angejitolea mhanga kuhakikisha Kenya imepata uhuru, kwa sababu yake mwenyewe na kizazi kijacho.

 Picha/ Sammy Waweru.
Ajuza Grace Njoki Mwangi maarufu kama Kanguniu, akiwa nyumbani kwake kijiji cha Ngunguru, Gathogorero, Kaunti ya Nyeri. Hutumia mkongojo baada ya kupata jeraha baya wakati wa vita vya MauMau.

Anasisitiza ni heri angesaliti nafsi yake, uhuru wa kujitawala urejelee Mwafrika na zaidi ya yote Mkenya. “Mwaka 1953 vita vilipochacha, maji yalizidi unga nilipoanza kusakwa. Sikuwa na budi ila kuokoa maisha yangu, kwa kutorokea Msitu wa Tumutumu,” Njoki anasimulia.

Ni katika harakati za kujinusuru, nyanya huyu aliuguza jeraha baya, kwa kudungwa na mwiba. “Jeraha hili si la leo, jana wala juzi. Ni la 1953 wakati nikitoroka kutafuta usalama, nilidungwa na mwiba ambao umesalia mguuni hadi kufikia sasa.

“Kiini changu cha kuchechemea na kutumia mkongojo kutembea kilitokana na tukio hilo,” akaambia Taifa Leo, wakati wa mahojiano nyumbani kwake kijiji cha Ngunguru, Mathira, Kaunti ya Nyeri. Alisema juhudi za kutafuta matibabu zimeambulia patupu, mwiba huo ukimkosesha usingizi.

“Nimekuwa nikihudhuria hafla za kitaifa, hasa maadhimisho ya Madaraka Dei na Sikukuu ya Mashujaa, ila mwaka huu sitaweza kwa sababu mguu uliopata jeraha maumivu hufufuka. Mara ya mwisho kuyahudhuria ilikuwa 2019,” akaelezea.

Picha/ Sammy Waweru.
Mzee James Njogu Getumbo, akiwa nyumbani kwake kijiji cha Gathondia, Kaunti ya Kirinyaga. Ni mmoja wa majasusi wa vita vya MauMau aliyeuguza majeraha mabaya.

Katika kijiji cha Gathondia, Kaunti ya Kirinyaga Mzee James Njogu Getumbo, ni mhasiriwa mwingine wa vita vya MauMau ambaye pia kumbukumbu za yaliyotukia zimekolea akilini.

Mzee Njogu ni jasiri, mkakavu na msemi wa mengi. Mateso na dhuluma alizopitia, wakati akitekeleza majukumu yake ya ‘ujasusi’ yangali mabichi mawazoni. Wajibu wa majasusi hasa ulikuwa kupasha ujumbe waliokuwa msituni usiku na mchana, katika mchakato mzima wa kuondoa serikali ya mkoloni.

Vilevile, ndio walitumika kupeleka vyakula, dawa, sigara, tumbaku na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

“Kwa sababu tulikuwa wadogo kiumri, na wengi wetu tulivalia sare za skauti, ilikuwa vigumu kutushuku. Pia tulikuwa tukisafirisha silaha kutoka eneo moja hadi lingine, kama vile panga, mikuki, na bunduki za kujitengenezea na zilizonyang’anywa askari waliouawa,” Njogu anafafanua.

Mwaka wa 1953, pamoja na vijana wenza, walibambwa na kusukumwa jela la Wamumu Approved, Kirinyaga, ambapo walisalia humo hadi Mei 1956.

“Tulipitia dhuluma, mateso na mahangaiko. Ninakumbuka kisa ambapo nilifungwa miguu na kuning’inizwa kwenye paa, kichwa kikielekezwa chini huku nikipokezwa kichapo,” Mzee Njogu akahadithia wakati wa mahojiano, akionyesha majeraha mabaya aliyouguza mgongoni na kwenye miguu.

Manusura hao wa MauMau, wanapotabasamu na kusimulia yaliyowafika, lao tu ni ombi kwa kiongozi wa nchi, Rais Uhuru Kenyatta awakumbuke, aafikie ahadi alizowapa.

Kwa Mzee Njogu, ingekuwa busara endapo barabara za miji na mitaa zingetambulika kwa majina ya mashujaa wa MauMau.

Katika ghala la nyanya Njoki, ana vipande kadha vya vibuyu (calabash), vilivyotumika kunywa uji, chai na pia maziwa, kati vya vinginevyo vikuukuu, vinavyomkumbusha enzi zile.

 

  • Tags

You can share this post!

Mpira wa vikapu kurejea viwanjani Juni 12-13, ratiba...

Malala haoni boriti katika jicho lake ila kwa mwingine