• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
FAUSTINE NGILA: Hatua ya Nigeria kuzima Twitter itaumiza wananchi

FAUSTINE NGILA: Hatua ya Nigeria kuzima Twitter itaumiza wananchi

Na FAUSTINE NGILA

KWA sasa, taifa la Nigeria linajipiga kifua jinsi lilivyozima mtandao wa kijamii wa Twitter wiki iliyopita, serikali ikidai kuwa mtandao huo unachafua sifa ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Isichojua Nigeria ni kwamba, kuwafungia nje wananchi wake kutumia Twitter kutawaumiza hata zaidi, hasa katika kipindi hiki ambapo biashara nyingi zinafanywa kupitia mitandao ya kijamii kama njia moja ya kudhibiti msambao wa virusi vya corona.

Kwa kufanya hivyo, taifa hilo, lenye watu zaidi ya milioni mia mbili, linajifungia lenyewe. Wananchi hawawezi tena kuwasiliana na mataifa mengine duniani kupitia Twitter kuhusu taarifa muhimu wala kupigia debe bidhaa zao.Wao pia hawawezi kung’amua kuhusu maendeleo yanayofanyika katika uchumi wa kidijitali, licha ya uwepo wa mitandao mingine kama Facebook na Instagram.

Ingawa si asilimia kubwa ya Wanigeria wanatumia Twitter, waliomo humo wanatambulika kote duniani kama wanaharakati wa mageuzi ya kisiasa, ambapo wamekuwa wakitumia mtandao huo kuikosoa serikali yao.

Kiuchumi, Nigeria ndilo taifa linalovutia uwekezaji mkubwa zaidi kutoka nchi za kigeni hasa katika sekta ya teknolojia, ambapo wabunifu wengi wamenufaika kwa kutangaza teknolojia zao kupitia Twitter – mtandao ambao wananchi milioni 40 wanamiliki akaunti katika taifa hilo.Hatua ya Twitter kufuta ujumbe wa Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari, ilichochea haya yote.

Lakini tukitazama taifa la Ghana ambako kuna uhuru wa kukosoa serikali, tunapata nchi iliyoimarika mno katika miaka ya hivi majuzi, inayofuata Kenya kwa uwezo wa kiteknolojia barani Afrika.Kutokana na hili, Twitter iliweka ofisi zake za Afrika jijini Accra, hatua ambayo huenda ikafuatwa na kampuni zingine za kiteknolojia kama Facebook – yenye ofisi zake za Afrika nchini Nigeria.

Pia, wawekezaji wa mataifa ya majuu huenda wakajiondoa kutoka soko la Nigeria ambalo sasa limepata sifa mbaya.Kufungwa kwa Twitter nchini humo, mwanzo, kutakuwa kazi ngumu. Wananchi pia wana mbinu zao za kupenya kuingia katika mitandao waliyokatazwa na serikali.

Tumejionea hayo katika nchi jirani ya Uganda ambako mtandao wa Facebook hadi sasa umezimwa, lakini wapenzi wa intaneti wanatumia mitandao ya kibinafsi (VPN) kuingia Facebook.Wanigeria hawana budi ila kupitia njia hiyo hiyo wanayotumia Waganda ili kuendeleza biashara zao na pia kupigania haki zao, na hilo litakuwa jambo ambalo serikali haitaweza kuzuia.

Nigeria inafaa kukumbuka kuwa uchumi wake umepata pigo la karne kutokana na janga la corona, na kuendelea kudidimisha juhudi za wananchi kujitafutia riziki mitandaoni ni tisho kwa maisha ya watu.Isitoshe, unapojaribu kuwahangaisha walipaushuru, maovu mengi hufanyika mitandaoni.

Usishangae kusoma habari kuhusu udukuzi katika mashirika ya serikali ya Nigeria kama njia moja ya kuilazimisha serikali kuondoa marufuku hiyo.Taifa hilo likumbuke kuwa doa kwa taifa moja barani Afrika huathiri sifa ya bara nzima, na kufanya wawekezaji waliopania kuwekeza mabilioni kusitisha mipango yao.

Nigeria ikomeshe udikteta wa mitandaoni na kuruhusu raia kufurahia matunda yanayoletwa na uwezo mkubwa wa intaneti.

You can share this post!

Malala haoni boriti katika jicho lake ila kwa mwingine

Likizo ni muhimu sana kwa afya ya akili ya wanafunzi