• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Mamia Mlima Kenya waombea corona itokomee

Mamia Mlima Kenya waombea corona itokomee

Na GEORGE MUNENE

MAMIA ya watu jana walifika katika msitu wa Mlima Kenya kuomba ili janga la corona ambalo limeua zaidi ya Wakenya 1,600 na kuathiri uchumi nchini litokomee mbali.

Waombaji hao kutoka sehemu mbali mbali nchini na ng’ambo, pia waliomba Mungu aingilie kati na kudumisha amani kutokana na kupanda kwa joto la kisiasa nchini.

Waombaji walisimama katika eneo la Samson Corner, kaunti ya Kirinyaga walipopiga magoti na kuomba kwa saa kadhaa wakitazama Mlima Kenya.

Baadhi yao walizidiwa na hisia na kulia wakiomba huku wakazi wakiwatazama.Kiongozi wao, Samuel Kamitha, aliwanyunyuzia maji matakatifu kuwakinga na mabaya wakielekea katika msitu kuomba Mungu.

“Sisi ni waombaji kutoka Kenya, Amerika na maeneo mengine. Tumeungana kwa maombi tukiwa na lengo moja,” alisema Bw Kamaitha.Waombaji hao walisema kwamba Covid 19 ni tishio kwa Wakenya.

“Hakuna lisilowezekana kwa Mungu wetu. Tunapoomba tukiwa mlimani, Mungu atasikia maombi yetu na kutuponya. Hata katika Bibilia watu walikuwa wakiomba kwenye milima na maombi yao yalijibiwa,” alisema Bw Kamitha.

Alisema kwamba joto la kisiasa nchini linaendelea kupanda kutokana na mchakato wa kubadilisha Katiba wa BBI na wanaomba ili Wakenya wasigawinyike.

Aidha, waliombea vijana wakisema wanateseka kwa kukosa ajira. Wakati mmoja, muombaji kutoka Amerika, Terry Fitzgerald, alitiririkwa na machozi alipoona Wakenya wakiwa wameungana kukabiliana na janga la corona kwa maombi.

“Tofauti na nchi yetu ambako watu weusi wanadhulumiwa na kubaguliwa, hapa Kenya watu wameungana hata na raia wa kigeni,” alisema huku akitokwa na machozi.

You can share this post!

Linturi alaumu Rais kwa kupuuza kilio cha Wakenya

CECIL ODONGO: Muungano wa Kalonzo hauna ushawishi kisiasa